Pambano Kali la Masumbwi

Hayawi hayawi mara huwa, ndivyo wanavyoweza kusema wapenzi wengi wa masumbwi duniani.

Deontay kumkabili Fury

Ni lile pambano la uzito wa juu duniani upande wa masumbwi lililoacha watu na fadhaa baada ya kutoka sare baina ya Deontay Wilder na Tyson Fury mnamo tarehe 1 Desemba, 2018. Yaaaah, ilikuwa ni sare ya alama 113 kila mmoja, tunaweza sema hakukuwa na mbabe siku hiyo.

Wapenzi tukawa na duku duku na shauku kuona lini litarudiwa. Hatimaye, Mungu si Athumani, ndiyo, Mungu si Athumani kwani pambano lenyewe ni alfajiri ya kesho tarehe 22 Februari, 2020 katika viwanja vya MGM Grand Garden huko Las Vegas, Amerika.

Ilikuwa ni bahati kwa sare ya Deonaty na Fury?

Kila mmoja anataka kumdhihirishia mwenziye kuwa ile sare ya kwanza aliipata kwa ngekewa tu au kwa bahati. Unajua kwanini wanasema hivyo? Jibu ni rahisi tu, kwa kuwa wote ni undefeated champion (mabingwa wasiowahi kupigwa).

Pia, wote wana sare moja ambayo waliipata kwenye pambano lao la kwanza. Hebu tazama makali yao hapa chini:

Deontay Wilder

Deontay Wilder

Huyu Deontay Wilder ni jitu haswa lenye futi 6.7, jeusi tii, hebu fikiria mtu aliyepigana mapambano 43, katoa sare moja tu. Kisha katika hayo 42, 41 kashinda kwa KO. Mwenyewe anajiita The Bronze Bomber, hilo neno Bronze lilitokana na kushinda medali ya Bronze kwenye Olympic.

Ila kwenye neno Bomber au Kiswahili, Bomba maana yake ni ngumi nzito. Ndiyo, ngumi nzito, muulize Dominic Breazale atakujibu kuwa hilo halina shaka kwani alikumbana nayo tena ndani ya round ya kwanza, akalala chini! Wazungu wanasema one punch knout out.

Kama kuna mwanamasumbwi alijuta kurudiana na Wilder basi ni Bermane Stiverne, alikutana na kichapo kitakatifu tena round ya kwanza ngumi zaidi ya 12 kichwani. Akaomba yaishe na refa hakuwa na hiyana akampa Wilder ushindi.

Hebu achana naye huyu Mmarekani tumkague Muingereza sasa:

Tyson Fury

Tyson Fury au The Gypsy King kama anavyojiita. Huyu ni mwamba mwenye urefu wa futi 6.9, mweupe pee, kama asili ya Waingereza, huyu jamaaa anajua kupigana. Haswa ana maujuzi ya kukwepa ngumi, swali hili ukimuuliza bondia Tom Schwartz atakujibu vizuri. Ndiyo, atakujibu kwani alirusha ngumi zaidi ya saba mfululizo na zote zikatoka patupu.

Pia, ana ujuzi wa kushambulia huku anamtafuta mpinzani, hata Klitschko atakuambia hivyo. Kimsingi jamaa ana uwezo wa kupambana katika round zote 12 huku akikufanya ufurahie kumtazama ndiyo maana ana mapambano 10 aliyomaliza round 12. Ndiyo maana Mike Tyson na Klitschko wamempa kura zao kuwa atashinda leo.

Tofauti ya Deontay Wilder na Tyson Fury ni nini hasa?

Tofauti iliyopo baina ya mabondia hawa ni kuwa Wilder anabutua (brutal fighting) wakati Fury anapigana.

Vipi Deontay Wilder angekuwa kibaka?

Kinachoniacha na furaha wakati nalingoja pambano hili ni kuwa wanaume hawa walichagua wawe mabondia na siyo vibaka. Hebu vuta picha Wilder angekuwa kibaka, ile unakata chochoro za uswazi tu unakuta na ngumi (punch au bomber) ya uso. Haaahaaa, kweli acha Mungu Aitwe Mungu.

Usiku wa kazi ulingoni

Fuatilia pambano uwanjani leo na moja kwa moja kwenye tovuti yetu!

Acha ujumbe