Senegal inakabiliwa na uwezekano wa kuwekewa adhabu na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya timu yao kuzua utata kwa kuondoka uwanjani wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya wenyeji Morocco.

Maandamano hayo makubwa yalichochewa na uamuzi wa penalti wa dakika za mwisho, hali iliyopelekea mchezo kusimama kwa muda kabla ya Senegal hatimaye kushinda katika muda wa nyongeza.
Tukio hilo lilitokea katika dakika ya nane ya muda wa nyongeza pale Morocco ilipopewa penalti baada ya mapitio ya VAR, muda mfupi baada ya bao la Senegal kufutwa.
Kocha mkuu Pape Thiaw aliwaongoza wachezaji wake kuondoka uwanjani kama ishara ya kupinga uamuzi huo, hatua iliyosababisha kucheleweshwa kwa mchezo kwa dakika 16 kabla ya kuendelea tena.
Brahim Diaz wa Morocco alikosa penalti hiyo, na Senegal wakaendelea kushinda mechi hiyo kwa bao la kushangaza la muda wa nyongeza lililofungwa na Pape Gueye.
Licha ya ushindi huo, sherehe za Senegal zinatarajiwa kufunikwa na hatua za kinidhamu.
Waandaaji wa mashindano hayo, CAF, wamelaani vikali tabia hiyo. Katika taarifa yao, shirikisho hilo lilisema:
“CAF inalaani tabia isiyokubalika ya baadhi ya wachezaji na maofisa wakati wa fainali ya TotalEnergies CAF Africa Cup of Nations Morocco 2025 kati ya Morocco na Senegal jijini Rabat jana usiku.”

“CAF inalaani kwa nguvu zote tabia yoyote isiyofaa inayotokea wakati wa mechi, hasa ile inayolenga waamuzi au waandaaji wa mchezo. CAF inapitia picha zote za tukio hilo na italifikisha suala hili kwa vyombo husika ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watakaobainika na hatia.”
Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Sadio Mané, alionekana kusita kujiunga na maandamano hayo, na baadaye alisema kuwa nchi yake ingekuwa “imekosea kabisa” kama isingemaliza mchezo.
Aliwaambia waandishi wa habari: “Ingekuwa aibu na jambo la kusikitisha kuona hali kama hiyo ikitokea. Hebu fikiria kwa sekunde moja tu kama tungeingia vyumbani na mechi ikaishia hapo. Nafikiri hilo lingeipa soka letu taswira mbaya. Nafikiri Afrika ya leo haistahili hilo.”
“Soka la Afrika limepiga hatua kubwa sana, na ushahidi ni kwamba linafuatiliwa kote duniani. Kwa upande wangu, nilifanya nilichopaswa kufanya. Nafikiri ingekuwa wazimu kutocheza mechi hii kwa sababu tu mwamuzi ametoa penalti na sisi tunaondoka uwanjani. Hilo lingekuwa jambo baya zaidi, hasa katika soka la Afrika. Afadhali nipoteze kuliko kuona mambo kama haya yakitokea kwenye soka letu.”
Kocha mkuu wa Senegal, Pape Thiaw, baadaye aliomba radhi kwa kitendo hicho. Akizungumza na beIN Sports, alikiri:
“Baada ya kutafakari, niliwaambia warudi (uwanjani) – wakati mwingine unaweza kuchukuliwa na hisia za papo kwa papo. Tunakubali makosa ya mwamuzi. Hatukupaswa kufanya hivyo, lakini tayari yameshatokea na sasa tunaomba radhi kwa soka.”


