Kombe la Shirikisho Barani Afrika limeendelea hapo jana kwa michezo kadhaa ambapo katika Dimba la Mkapa, Yanga ilikuwa ikimenyana dhidi ya TP Mazembe na kufanikiwa kuichakaza kwa mabao 3-1.
Mpaka kufikia kipindi cha mapumziko Yanga walikuwa wanaongoza mabao mawili ambayo yalifungwa na Kennedy Musonda pamoja na Mudathiri Yahaya na kuwafanya Mazembe kuchanganyikiwa mapema.
Vijana hao wa Nabi waliingia mchezoni wakihitaji ushindi pekee baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao mawili kwa bila.
Lakini nao Mazembe ambayo yupo mchezaji wa zamani ya Young Africans Mukoko Tonombe walipata bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa faulo kipindi cha pili, kabla ya Tuisila Kisinda kupachika bao la ushindi wa moja kwa moja dakika za jioni kabisa za mchezo.
Baada ya ushindi huo timu ya wananchi wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo huku US Monastir wakiwa vinara wa kundi wakiwa na pointi nne.
Yanga mechi inayofuata itakuwa ya Ligi ambayo watamenyana dhidi ya KMC kabla ya kuja kukiwasha dhidi ya Real Bamako kwenye mchezo wa tatu.