Rekodi Kali za Simba na Yanga

Jumapili, Oktoba 23, 2022, watani wa jadi wa jiji la Dar es Salaam na hapa Tanzania, Yanga na Simba watakutana katika mchezo wa kwanza wa Ligi kuu ya NBC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kama ilivyo kwa mechi za namna hiyo maeneo mengine duniani, mechi za Yanga na Simba zimekuwa zikizalisha rekodi na kumbukumbu ambazo kwa kiasi kikubwa huchangia kufanya mechi kuonekana ya kipekee.

 

Rekodi Kali za Simba na Yanga

Makala hii inakuletea rekodi kadhaa zilizowekwa na mechi baina ya Simba na Yanga katika mashindano mbalimbali ambazo zimechezwa ndani ya kipindi cha miaka 12 ya hivi karibuni.

MABAO 7 MECHI MOJA

Mpaka sasa kwenye muda wa miaka 12 iliyopita mchezo wa Simba na Yanga uliozalisha mabao mengi ni ule wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2009/2010 uliochezwa Aprili 18, 2010 ambao yalizalishwa jumla ya mabao saba.

Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-3. Mabao yake yakipachikwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyefunga mawili, huku mengine yakiwekwa kimiani na Uhuru Selemani na Hillary Echesa.

Mabao matatu ya Yanga yalifungwa na Jerry Tegete aliyepachika mawili, huku lingine likifungwa na Athuman Idd ‘Chuji’.

MABAO SAWA KILA KIPINDI

Ni nadra sana kwa idadi sawa ya mabao kufungwa katika kila kipindi katika mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba. Hata hivyo rekodi hiyo iliwekwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 uliopigwa Oktoba 20, 2013 na timu hizo kila moja ilishinda kipindi kimoja, moja kipindi cha kwanza na mwingine kipindi cha pili.

Timu hizo kila moja ilishinda mabao matatu, Yanga ikifanya hivyo kipindi cha kwanza na Simba kupata yake kipindi cha pili na mechi kumalizika kwa sare ya 3-3.

Yanga ilitangulia kupata mabao yake kupitia kwa Mganda Hamis Kiiza aliyepachika mawili huku Mrisho Ngassa akifunga moja na mashabiki wake kuamini walikuwa wakipata ushindi mnono na pengine kulipa kiasi cha mabao 5-0 walichopigwa misimu miwili iliyopita.

Hata hivyo katika kipindi cha pili kilikuwa cha Simba ambayo ilisawazisha mabao yote matatu kupitia kwa Joseph Owino, Bertram Mwombeki na Gilbert Kaze.

BAO LA JIONI

Mchezo wa Fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati wa Julai 10,2011 uliochezwa katika Uwanja wa Mkapa ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0, ndio ambao umeandika historia ya bao la dakika za mwisho zaidi pindi timu hizo zilipokutana ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Bao hilo lilifungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Kenneth Asamoah katika dakika ya 109 akimalizia krosi ya Rashid Gumbo katika mchezo huo ulichezwa kwa dakika 120.

KONA GOLI

Katika kipindi cha miaka 12, mchezo wao wa Oktoba Mosi, 2016 unakumbukwa zaidi kutokana na bao la aliyrekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya alilofunga katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 .Yanga wakiwa na imani ya kuendeleza ubabe wao kwa watani wao, kwani ilikuwa imetoka kuinyoa timu hiyo mara mbili kwa mabao 2-0, hasa baada ya kutangulia kupata bao lililozua utata la Amissi Tambwe.

Tambwe alifunga bao lililoonekana la kuutengeneza kwa mkono na kusababisha aliyekuwa nahodha Jonas Mkude kuonyeshwa kazi nyekundu. Hata hivyo dakika zikiyoyoma, Kichuya aliyekuwa moto na mwiba mchungu enzi hizo alipiga mpira wa kona ulioingia moja kwa moja golini.

KIPA KUTUPIA NYAVUNI

Katika kipindi cha miaka 12 ya hivi karibuni, Juma Kaseja ndiye kipa pekee aliyefunga bao katika mechi zinazokutanisha watani hao wa jadi, akifanya hivyo katika pambano la Mei 6, 2012 wakati Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 5-0 mbele ya Yanga. Kaseja alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti akifuata nyayo iliyowahi kufanywa na aliyekuwa pia kipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ aliyefanya hivyo kwenye mchezo wa Simba na Yanga wa Ligi mwaka 1985.

USHINDI MKUBWA

Kipigo cha mabao 5-0 ambacho Simba ilikitoa kwa Yanga, Mei 6, 2012 ndio kikubwa zaidi kwa timu moja kukipata katika mechi za watani wa jadi ndani ya kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni. Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi aliyepachika mawili, Felix Sunzu, Juma Kaseja na marehemu Patrick Mafisango.

Hicho kilikuwa ni kipigo cha pili kwa Yanga kutoka kwa watani wao, kwani tayari walikuwa na deni la kulipa 6-0 walichopewa Julai 19, 1977, walipokuwa wakipiga kisasi cha kupigwa mabao 5-0 na Yanga kwenye mchezo wao uliochezwa Juni 1, 1968.

MAREFA SITA

Mechi ya kwanza ya Watani wa Jadi kuchezeshwa na marefa sita (6) ni ile ya Machi 8, 2020 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na kabla ya hapo mechi hizo hazikuwahi kuchezeshwa na idadi hiyo ya waamuzi. Waamuzi hao sita walikuwa ni Martin Saanya aliyekuwa katikati, na washika vibendera Mohamed Mkono na Frank Komba huku mwamuzi wa nne akiwa ni Elly Sasii.

Pia kulikuwa na marefa wawili waliosimama nyuma ya magoli. Simba ilifungwa bao 1-0.

Katika kipindi cha hivi karibuni Yanga wamekuwa na rekodi nzuri mbele ya watani wao Simba kwani mara ya mwisho Simba kumfunga Yanga ni mwaka 2019 goli la kichwa la Medie Kagere akimtungua Kipa Ramadhan Kabwili baada ya hapo imebaki historia.

Acha ujumbe