Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Miguel Gamondi ameongeza nyota wawili kutoka kikosi cha Serengeti Boys kwenye kikosi kitakachocheza mechi mbili za kirafiki za kalenda ya FIFA mwezi Juni mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni Luqman Mbalasalu pamoja na Kassim Juma ambao kwa sasa wako nchini Morocco kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17).
Bila kusahau meridianbet ndio wakali wa ODDS KUBWA, Machaguo zaidi ya 1000 na kila kitu ukitakacho. Bashiri kijanja hapa
Kupitia taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wachezaji hao watajiunga na kambi ya Taifa Stars mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali wa AFCON U17 dhidi ya Senegal utakaochezwa Juni 2, 2026 nchini Morocco. Hatua hiyo inaonesha imani kubwa ya benchi la ufundi kwa vijana hao wanaofanya vizuri kwenye mashindano hayo ya Afrika.
“Kocha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Miguel Gamondi ameongeza wachezaji wawili kutoka Timu ya Taifa U17 (Serengeti Boys), Luqman Mbalasalu na Kassim Juma kwa mechi mbili za kirafiki kwenye kalenda ya FIFA,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya TFF.
Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Uganda Juni 5 kabla ya kushuka dimbani tena Juni 9 dhidi ya Rwanda. Michezo yote miwili itapigwa jijini Marrakech, Morocco ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu hiyo kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.
Kwa upande mwingine, wachezaji wengine walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars tayari wameanza kuripoti kambini jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya mechi hizo. Ujio wa vijana kutoka Serengeti Boys unatajwa kuongeza ushindani na nguvu mpya ndani ya kikosi hicho cha Miguel Gamondi.


