Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) limemteua tena Roberto Mancini kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italia kwa kipindi cha pili, baada ya mpango wa kumkabidhi nafasi hiyo Andrea Pirlo kuvunjika kufuatia changamoto za kiutawala na kimaadili.
Taarifa zinaeleza kuwa Andrea Pirlo alikuwa tayari amefikia makubaliano ya mdomo kuiongoza Italia hadi mwaka 2030. Hata hivyo, Rais wa FIGC, Giovanni Malagò, alisimamisha mchakato huo kutokana na utata ulioibuliwa na nafasi ya Pirlo kama balozi wa kimataifa wa kampuni ya kubashiri ya Urusi, Fonbet, jambo lililomlazimu kujiondoa kwenye mchakato wa uteuzi.
Hatua hiyo ilisababisha msukosuko ndani ya FIGC, ambapo Mkurugenzi wa Ufundi Paolo Maldini pamoja na mshauri wa kimkakati Leonardo Araujo walijiuzulu wakipinga uamuzi huo. Wawili hao walikuwa mstari wa mbele kushinikiza Pirlo apewe nafasi hiyo baada ya makocha Pep Guardiola na Carlo Ancelotti kukataa ofa ya kuinoa Italia.
Kutokana na muda kuwa mfupi kuelekea ratiba ya mechi za kimataifa, viongozi wa FIGC walimgeukia Roberto Mancini, ambaye alikuwa hana klabu baada ya kuondoka Al-Sadd ya Qatar. Mancini aliwahi kuinoa Italia kati ya mwaka 2018 na 2023, akiiwezesha kutwaa ubingwa wa Euro 2020 na kuweka rekodi ya kutopoteza mechi 37 mfululizo kabla ya kujiuzulu mwaka 2023.
“Sambamba na kurejea kwa Roberto Mancini, Claudio Ranieri ameteuliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa Ufundi wa FIGC akichukua nafasi ya Paolo Maldini. Kazi ya kwanza ya Mancini itakuwa kuiandaa Italia kwa mechi za UEFA Nations League mwezi Septemba dhidi ya Ubelgiji, Uturuki na Ufaransa, huku lengo kuu likiwa ni kuirejesha Azzurri kwenye michuano ya Dunia la mwaka 2030.”


