UONGOZI wa Azam FC umemsajili beki wa kulia kutoka Ruvu Shooting, Nathaniel Chilambo kwa mkataba wa mwaka mmoja. 
Chilambo alikuwa kwenye kiwango bora kwa msimu wa 2021/22 akiwa na kikosi cha Ruvu Shooting kiasi cha kuhusishwa na baadhi ya klabu zikiwemo Simba na Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Azam FC kupitia ukurasa wa mtandao wao wa kijamii ilieleza kuwa “Tunayo furaha kuwataarifu kuwa tumeingia mkataba wa mwaka mmoja na beki wa kulia, Nathaniel Chilambo, kutoka Ruvu Shooting.
“Chilambo amesaini mkataba huo mbele ya mmiliki wa timu, Yusuf Bakhresa na Afisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin wenye kipengele cha kuongeza baada ya miezi sita kutokana na kiwango atakachokionyesha.
“Beki huyo (19), anayetumia miguu yote miwili kwa ufasaha, mwenye uwezo pia wa kucheza beki ya kushoto, amekuwa na kiwango bora kabisa msimu uliopita.
“Azam FC tumekuwa mstari wa mbele wa kukuza soka la vijana na kuheshimu vipaji vya wachezaji wazawa, tunaamini Chilambo atakuja kuwa msaada mkubwa kwenye kikosi chetu katika eneo hilo.”

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa