Kibadeni Afichua Kilichonyuma ya Hat-trick yake

MCHEZAJI nguli wa zamani wa Simba Abdallah Kibadeni amesema kuwa kinachofanya rekodi yake ya kufunga mabao matatu kwenye mechi ya Simba na Yanga isivunjwe ni kukosekana kwa wachezaji wenye roho ngumu ya kutaka kufanikiwa kupitia mechi hiyo.

Kibadeni amesema yeye alifanikiwa kuweka rekodi hiyo kwa sababu alikuwa na uchu wa kutaka kuonyesha kitu kwenye kila mchezo ambao alikuwa anacheza na wakati wanajiandaa kucheza na Yanga alifanya mazoezi ya ziada ambayo yalimpa urahisi wa kutoboa.

Kibadeni alisema kuwa yeye alikuwa anafanya mazoezi zaidi ya kawaida kila inapokaribia mechi ya Simba na Yanga na alikuwa na utaratibu wa kufanya hivyo kwenye kila mechi ambayo alikuwa anataka kuacha alama jambo ambalo vijana wa sasa hawafanyi.

Kibadeni Afichua Kilichonyuma ya Hat-trick yake

“Siku mbili kabla ya ile mechi ambayo nilifunga mabao matatu, tulifanya mazoezi usiku na kwenye uwanja ambao haukuwa na taa. Kilichofanyika kila mtu mwenye gari aliwasha taa za gari yake likiwemo la kwangu ili kuweza kupata mwanga.

“Tulifanya sana mazoezi usiku ule na hiyo ilitokana na hasira ya kuzomewa na mashabiki wa Yanga baada ya sisi Kwenda kutazama mechi yao ambayo walishinda mabao 4-0. Wao wakaamini hata sisi watatufunga.

“Binafsi nikasema lazima nifanye kitu kwenye mchezo huo na kweli ikawa hivyo. Tukawafunga Yanga mabao 6-0 na mimi nikafunga mabao matatu,” alisema.

Huo ulikuwa ni mchezo wa ligi ambao ulichezwa mwaka 1977 na Kibadeni kuweka rekodi ya kufunga Hat-trick inayodumu hadi leo ambapo alisema itachukua muda mrefu zaidi rekodi yake hiyo kuvunjwa.

Acha ujumbe