Anthony Joshua alimshinda Jake Paul kwa knockout (KO) katika raundi ya sita ya pambano lililofanyika Miami, ingawa pambano hilo kwa ujumla halikuwavutia wengi. Katika mapambano hayo, Joshua alimwangusha Paul chini mara nne kabla ya mwamuzi Chris Young kusitisha pambano hilo dakika 1:31 ya raundi ya sita. Licha ya ushindi huo, wengi waliona huu kuwa ni moja ya mapambano ambayo Joshua hakuonekana kuwa katika kiwango chake bora kama bondia wa kulipwa.

Tangu kengele ya mwanzo, Jake Paul alionekana kukimbia na kuepuka mapambano ya karibu, jambo ambalo kwa hakika lilikuwa wazo sahihi kwake. Pambano lilifanyika kwenye ulingo mkubwa wa futi 22 kwa 22, hali iliyompa Paul nafasi ya kutumia kasi na harakati zake kukwepa mashambulizi ya Joshua, ambaye ni bondia mwenye uzoefu mkubwa na nguvu. Hata hivyo, mkakati huo ulimchosha Paul haraka.
Kufikia raundi ya nne, kasi ya pambano ilianza kushuka na wakati mwingine ilionekana kama mchezo wa kuchekesha. Paul, akiwa amechoka, alianza kujirusha mara kwa mara kuelekea kwa Joshua kana kwamba alikuwa akijaribu kumshawishi afanye makosa au faulo. Mbinu hiyo haikufanikiwa, kwani Joshua alianza kumpata kwa mapigo safi yaliyosababisha Paul kuanguka mara kadhaa, hadi mwamuzi alipoamua kusitisha pambano hilo.
Licha ya ushindi na knockdowns alizopata, ni vigumu kwa timu ya Anthony kuona mambo mengi ya kujivunia kutokana na pambano hili. Kulikuwa na nyakati ambazo ilionekana kana kwamba Antony alikuwa akijizuia au hakuwa akitumia uwezo wake wote. Hakufanana kabisa na yule bondia aliyepambana na Francis Ngannou mwaka 2024 na kuonyesha wazi kwamba bingwa huyo wa zamani wa UFC hakuwa na nafasi kwenye ulingo wa ndondi dhidi yake.

Ni kweli kwamba Jake Paul alifanya pambano liwe gumu kwa kukimbia na kutumia ulingo mkubwa, lakini kwa bondia mwenye uzoefu, historia na uwezo wa Joshua na kwa kuzingatia kuwa ana umri wa miaka 36 ambao bado si mkubwa sana wengi walitarajia aonyeshe kiwango bora zaidi. Ingawa ni vigumu kusema kwamba Paul alikuwa mpinzani mwenye ushindani wa kweli, ushindi wake wa kimaadili ni kwamba aliweza kudumu hadi raundi ya sita, jambo ambalo wapinzani wengi wa Joshua hawajawahi kufanikiwa.
Baada ya pambano, Anthony mwenyewe alikiri kwamba hakutoa kiwango chake bora. Alisema lengo lake lilikuwa ni kumkaba Jake Paul, kumzuia asikimbie na kumuumiza mapema, lakini mpango huo ulichukua muda mrefu zaidi ya alivyotarajia. Hata hivyo, alieleza kuwa hatimaye mkono wake wa kulia ulipata shabaha na kumaliza pambano.



