Arsenal imepata pigo la mapema baada ya winga wake, Christos Tzolis, kuumia akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Ugiriki katika mchezo wa UEFA Nations League dhidi ya Uholanzi. Tzolis, mwenye umri wa miaka 24, alianza mchezo huo lakini alidumu uwanjani kwa dakika 18 pekee kabla ya kulazimika kutolewa kutokana na jeraha.
Tzolis alianza mchezo kwa kasi na alikaribia kuifungia Ugiriki dakika ya 13, hata hivyo bao hilo lilikataliwa baada ya mshambuliaji Vangelis Pavlidis kuonekana kuingilia mchezo akiwa katika nafasi ya kuotea. Winga huyo alikuwa akionekana kuwa tishio upande wa kushoto, akimpa wakati mgumu beki wa Uholanzi, Denzel Dumfries.
Hata hivyo, dakika tano baadaye hali ilibadilika baada ya Tzolis kuanguka uwanjani huku akishikilia sehemu ya nyuma ya paja lake la kulia. “Tzolis alionekana kupata maumivu makali na madaktari wa timu ya Ugiriki walifika haraka kumfanyia vipimo,” huku mchezaji huyo akionekana kuvunjika moyo na kufunika uso wake kwa mikono.
Kocha wa Ugiriki, Ivan Jovanovic, hakutaka kuhatarisha hali ya mchezaji huyo na alifanya mabadiliko mapema, akimtoa Tzolis na nafasi yake kuchukuliwa na Giorgos Masouras. Kwa sasa, Arsenal inasubiri taarifa zaidi kuhusu ukubwa wa jeraha hilo pamoja na muda ambao mchezaji huyo anaweza kuwa nje ya uwanja.
Jeraha hilo limeongeza wasiwasi ndani ya Arsenal kutokana na Tzolis kuanza msimu kwa kiwango kizuri tangu alipowasili klabuni hapo akitokea Club Brugge kwa ada ya rekodi ya pauni milioni 35. Klabu hiyo sasa inasubiri tathmini kamili ya kitabibu ili kubaini kama jeraha hilo litamuathiri katika ratiba ya michezo ijayo.


