Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coventry City katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England umeonyesha kuwa mabingwa hao bado wana njaa ya kutwaa mataji. Arsenal ilianza utetezi wa ubingwa kwa kiwango bora, ikipata mabao kupitia Kai Havertz, Bukayo Saka na Martin Odegaard kwenye Uwanja wa Emirates.
Arteta amefurahishwa na namna wachezaji wake walivyoingia kwenye mchezo kwa nguvu, wakitawala mchezo na kutumia presha kubwa kuinyima Coventry nafasi ya kujenga mashambulizi. “Kwa mtazamo wangu wanaonekana vilevile kama msimu uliopita. Nilichowaambia ni kuonyesha hamu zaidi na kuhakikisha tunastahili kuwa bora kuliko kila mtu mwingine. Kulikuwa na mambo mengi ya kupendeza katika mchezo huu. Ilikuwa ni ushindi mzuri, lakini pia namna tulivyoanza ilikuwa ya kuvutia,” alisema Arteta.
Kocha huyo pia amesifu muunganiko uliopo kati ya wachezaji wake, huku mchezaji mpya Christos Tzolis akifanya vizuri katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu tangu alipojiunga akitokea Club Brugge. “Tulikuwa bora sana, tulikuwa na muunganiko wa ajabu na tulikuwa sahihi sana katika kutumia mpira. Wachezaji walipaswa kutumia nafasi zao kwa ufanisi na walifanya hivyo leo. Walionekana kuungana vizuri na kucheza kwa malengo,” aliongeza Arteta.
Kuhusu usajili wa beki Ezri Konsa kutoka Aston Villa, Arteta amesema mchezaji huyo ataongeza ubora na ushindani kwenye safu ya ulinzi, lakini hakubaliani na mtazamo kwamba Arsenal tayari ni bora kuliko wapinzani wao wote. “Hapana, kwa sababu ukiangalia vikosi vya baadhi ya timu, vina ubora mkubwa na ni vikubwa kuliko chetu. Tunachotaka ni kuendelea kuboresha na kuelewa ni wachezaji gani wanaweza kutuongezea nguvu. Ezri ni mchezaji tunayempenda sana kwenye safu ya ulinzi. Tumemsajili beki bora mwenye tabia nzuri, hivyo ninafurahi sana,” alisema.
Nahodha Martin Odegaard amesema Arsenal imepata mwanzo bora kabisa, huku akisisitiza kuwa timu hiyo haitaki kutazama nyuma bali inapanga kupigania ubingwa tena. “Ni mwanzo mkamilifu. Mabao matatu na kutoruhusu bao. Tulikuwa imara sana. Hatuhisi kwamba tunapaswa kutetea chochote; tunataka kufanya hivyo tena, huo ndio mtazamo wetu. Msimu uliopita umekwisha, sasa tunataka kurudia na kupigania taji tena,” alisema Odegaard. Kwa upande mwingine, kocha wa Coventry, Frank Lampard, alikiri Arsenal ilikuwa bora na timu yake imepata somo muhimu kutokana na mchezo huo.


