Kocha wa Mamelodi Sundowns, Miguel Cardoso, amegoma kuweka wazi hali ya majeruhi wa kikosi chake kuelekea fainali ya MTN8 dhidi ya Orlando Pirates itakayochezwa Jumamosi. Wachezaji Tebogo Mokoena, Aubrey Modiba na Bathusi Aubaas walirejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Afrika Kusini wakiwa na changamoto za majeraha.
Cardoso amesema klabu haitachukua hatari kwa kumlazimisha mchezaji yeyote kucheza kabla ya kuwa tayari, huku akieleza kuwa madaktari bado wanaendelea kutathmini hali zao. Kauli hiyo pia inawaacha Pirates bila uhakika kuhusu wachezaji hao watatu kama watakuwa sehemu ya kikosi cha Sundowns kwenye mchezo huo muhimu.
“Ni muhimu kufahamu kwamba hatutahatarisha afya ya mchezaji yeyote. Wachezaji walifika jana na tumewafanyia tathmini. Madaktari wamepata mawasiliano yao ya kwanza nao, hivyo tusubiri tuone watakavyoitikia mazoezi tunayowapa,” Cardoso alisema.
Licha ya fainali hiyo kuwa na zawadi ya kwanza ya Rand milioni 10, Cardoso amesema pia anazingatia ratiba ya michezo inayofuata, ikiwemo mchezo wa Premiership dhidi ya Richards Bay na kisha hatua ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete ya Angola. Sundowns haijatwaa MTN8 tangu mwaka 2021, huku Orlando Pirates ikishinda kila fainali iliyochezwa tangu wakati huo.
Wakati huo huo, Cardoso amefichua kuwa amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na Sundowns, akisema anafurahia mazingira ya klabu hiyo na anahisi kuheshimiwa. “Nina mkataba wa muda mrefu na nina furaha sana. Kwa kocha, jambo muhimu zaidi ni kufanya kazi na watu wanaokutaka kweli. Nimehisi kuheshimiwa kama mtu na ninashirikiana na familia yenye maadili yanayofanana na yangu, jambo ambalo ninalishukuru sana,” alisema.


