MAMBO ni moto kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2022/23 ambapo tayari
ratiba ya msimu mpya imewekwa hadharani huku mchezo wa kwanza wa dabi ya
Kariakoo unaozikutanisha timu za Simba na Yanga ukitarajiwa kupigwa
Oktoba 23, mwaka huu.

Jana Jumatano Uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ulitangaza
rasmi ratiba hiyo ambapo michezo ya mzunguko wa kwanza inatarajiwa
kuanza kupigwa Agosti 15, mwaka huu ambapo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu
Bara Yanga wanatarajia kuanzia ugenini dhidi ya Polisi Tanzania Agosti
16, mwaka huu.

Simba na Azam wao wanatarajia kuanzia michezo yao ya mzunguko wa kwanza
nyumbani ambapo Simba watacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Geita Gold,
huku Azam waliomaliza kwenye nafasi ya tatu wakianzia nyumbani dhidi ya
Kagera Sugar.

Michezo ya kufungia msimu wa 2022/23 inatarajiwa kupigwa Mei 27, mwaka
2023 na michezo ya kwanza ya mtoano ‘Play Off’ ikipigwa Mei 31, na
michezo ya marudiano itapigwa Juni 3, mwaka 2023.

CEO wa TPLB, Almasi Kasongo alisema: “Tunatarajia kuwa na michezo 240
ya mizunguko 30 kwa msimu mpya wa 2022/23 ambapo 120 ni michezo ya
nyumbani na 120 ya ugenini, michezo ya mzunguko wa kwanza inapigwa
Agosti 15, mwaka huu na michezo ya mzunguko wa mwisho itachezwa Mei 27,
mwaka 2023.

“Kutakuwa na mapumziko 17 ya kupisha shughuli mbalimbali kama
mashindano ya ndani na kimataifa na pia Shughuli ya Sensa na mchezo wa
dabi ya kwanza utafanyika Oktoba 23, mwaka huu saa 11:00 kwenye Uwanja
wa Mkapa, Dar es Salaam.”

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa