Kipa wa Liverpool, Alisson Becker, ametozwa faini ya pauni 8,000 ($10,800) na Shirikisho la Soka England (FA) kutokana na tabia yake baada ya mchezo dhidi ya Nottingham Forest uliomalizika kwa sare ya 2-2 katika Ligi Kuu England mwezi uliopita.
Tukio hilo lilitokea baada ya Alisson kutoridhishwa na namna ubao wa kielektroniki wa mabadiliko ulivyocheleweshwa wakati Nottingham Forest ilipokuwa ikifanya mabadiliko matatu kwa wakati mmoja. Kipa huyo mwenye umri wa miaka 33 alipewa kadi ya njano baada ya kumlalamikia mwamuzi kuhusu tukio hilo.
Baada ya mchezo kuendelea, Forest ilifanya shambulizi la haraka kupitia Neco Williams, ambaye aliingia kwenye eneo la hatari la Liverpool na kuangushwa na Alisson. Tukio hilo lilipelekea Forest kupata penalti na kufanikiwa kuongoza kwa mabao 2-1, kabla Liverpool kusawazisha na kuambulia sare ya 2-2.
Baada ya filimbi ya mwisho, Alisson alionekana akipita eneo la handaki akiwa karibu na ubao wa mabadiliko uliokuwa umewekwa chini. Video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha kipa huyo akiuchezea kwa teke ubao huo, ambao ulidaiwa kuharibika kutokana na tukio hilo.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, msemaji wa FA alisema: “Ilidaiwa kuwa kipa huyo alitenda kwa namna isiyofaa katika eneo la handaki baada ya filimbi ya mwisho. Alisson Becker baadaye alikubali tuhuma hizo na kupokea adhabu ya kawaida.” Liverpool kwa sasa inaendelea na maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Fulham utakaochezwa Jumamosi.


