Pale mjini Shinagawa Nchini Japan wanajivunia mzee mmoja aitwaye Kurosawa Akira mtayarishaji wa Filamu mwenye tungo makini za Maisha, Yeye aliwahi kusema
‘Man is a genius when he is dreaming.” Mtu hutimamuka akiwa usingizini.
Yes, keti chini ewe Gael Bigirimana mume wa Mrembo Natalia Leigh, Nisikilize kwa makini kidogo. Najua Mpaka sasa umeshapata picha ya Ligi yetu, Huku kwetu Viatu vinagusa sana ngozi za miguu ya wapinzani. Hii ndiyo ligi inayohusudu nguvu na maarifa.

Usingizi haujawahi kuisha ewe Gael Bigirimana mwana wa Mzee Bigirimana wa pale Bujumbura, Amka sasa kwenye kitanda chenye godoro zito la GSM, Amka uwapeleke wananchi kwenye hekaya lako la Newcastle ya England, amka uwakumbushe mema yako.
Imani ya wananchi wengi ni kwamba unaweza wakumbusha zile pasi za Babu Chuji mbele ya Anko Ngasa wakati Ule, pengine ukawarudisha enzi za mbrazil Coutinho aliyeng’ara mpaka CCM Kirumba Mwanza, Amka uutambarize mpira kama ulivyoutambariza pale Stade Prince Louis Rwagasore Kwenye baraka za wazee wako.

Gael Bigirimana Bado miguu yako haijazungumza na wananchi, Bado kichwa chako hakijawaliwaza wananchi, bado jasho lako halijawakosha wananchi, Amka sasa Gael, amka kitandani Mwamba, amka ewe mfalme, usisubiri kitanda chako kitiwe Maji ili uamke, amka mwenyewe muafrika uliyeng’ara Ulaya.
Ukisibiri embe iive, Aucho anazidi kula na Chumvi.
Imeandikwa na Abdulazeez Kipanduka
Unaweza kutazama video za uchambuzi wa michezo na matukio kwa kugusa Video Hii