Kocha mkuu wa klabu ya Inter Milan Simone Inzaghi amekiri kuwa kibarua chake kipo hatarini kufuatia kipigo cha mabao 2-1 ambacho yeye anaamini hakustahili kupata kipigo hicho huku akiwa ni mwenyeji wa mchezo huo dhidi ya Roma.
Kupoteza huko kulihitimisha mfululizo wa ushindi mara saba mfululizo kwa Inter wakiwa San Siro kwenye Ligi lakini, licha ya matokeo hayo, Inzaghi anaamini kuwa kiwango hicho kilikuwa kizuri zaidi walichoonyesha msimu huu.
“Ni kushindwa tusiostahili kabisa. Ulikuwa mchezo wetu bora zaidi wa msimu huu na tumetoka na matokeo ambayo yanachoma na kuumiza,” aliiambia DAZN.
Inzaghi alisema lazima wafanye vya kutosha, ambapo kwa sasa hawafanyi vizuri na anasikitika kupoteza mchezo huo wakiwa nyumbani mbele ya mashabiki ambao wanawaunga mkono. Kipigo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Inter kwenye Serie A, huku kikosi cha Inzaghi kikipoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita, na amekiri kuwa nafasi yake iko hatarini.
Inter wanakabiliwa na mtihani mgumu ambapo watakutana na FC Barcelona siku ya Jumanne ambapo Simone hatarajii mshambuliaji wake Romelu Lukaku kurejea uwanjani kwenye mchezo huo.