Msuva Atoa Mazito

BAADA ya kushinda kesi dhidi ya klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, Simon Msuva amefunguka mazito ambayo alikumbana nayo akiwa huko.

Msuva amesema kuwa “Nipo hapa kwa niaba ya wachezaji wenzangu ambao walipitia mengi kwenye safari yao ya soka inawezekana wao walishindwa kuzungumza lakini mimi nimeweza kujitokeza na kuongea.

“Nimepitia mengi sana nikiwa Morocco ambapo ilifikia wakati nilikosa hela ya kulipia maji, nikaenda kwa rafiki yangu ambaye alikuwa mji mwingine nikaenda kukaa huko ambapo nilikuwa natokea huko kwenda mazoezini.

“Hela ilizuiliwa haikuingia kwenye kadi yangu ndio iliyosababisha hayo yote kutokea lakini nawashukuru sana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwa ajili ya sapoti yao waliyonipa mpaka kufikia hapa.”

“Pia nawashukuru sana watanzania wote, waandishi pamoja na wanasheria walionisaidia mpaka nafanikiwa kushinda kesi hii, kwa hiki kilichonitokea nimejifunza mengi sana na hata nikipata timu nyingine nitausoma vizuri mkataba wangu.

“Kuna kipindi sikuwa sawa kisaikolojia lakini nawashukuru viongozi wa TFF ambao waliona nafaa kuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa japo wengi waliona sifai ila nadhani nilitoa mchango wangu kwenye timu.”

Kwa upande wa mwanasheria wa Simon Msuva, Yasmin Razack amesema kuwa “Tulifanya kazi hii ya Msuva kuanzia mwezi disemba mwaka jana ilikuwa ni ngumu sana kutokana na aina ya mkataba aliokuwa amesaini.

“Tumekuwa tukishughulikia kesi kama hizi kwa wachezaji wakubwa kama vile Yaya Toure lakini wengi ambao tunawasaidia wanatoka Afrika na wanakumbana na hili kwani wanasaini mikataba ambayo hawaelewi lugha inayotumika pale ukiangalia kwa upande wa Msuva yeye mkataba wake uliandikwa kwa lugha ya kifaransa.

“Ndani ya masaa 48 Tanzania utajua Msuva anapoenda kwa sasa anamalizia vipimo tu lakini sio klabu za Simba na Yanga.”

“Na kwa sasa tuna kesi ya Mwanahamis Omary ambaye yupo Tanzania na alikuwa amekata tamaa kabisa lakini tunataka kumsaidia hivyo ningewaomba wachezaji wa kitanzania wawe na wanasheria ambao watawasaidia katika masuala ya sheria.”