RAIS wa Yanga, Eng Hersi Said ameweka wazi kuwa hawana presha yoyote na mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, hasa kutokana na mipango thabiti waliyoiweka na ubora wa wachezaji ambao wanakamilisha usajili wao mpaka sasa.

Yanga mpaka jana Jumanne mchana walikuwa wamekamilisha usajili na kuwatangaza mastaa wapya wanne ambao ni Lazarus Kambole, Bernard Morrison, Gael Bigirimana na Joyce Lomalisa ambao wanatazamiwa kuibeba kwenye mashindano ya kimataifa.

Yanga ambao wamefanikiwa kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita wanatarajiwa kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo wataanzia hatua ya awali kwa michezo itakayopigwa kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.

Hersi alisema: “Tunafahamu kuwa mashindano ya kimataifa yanahitaji nguvu kubwa na muda wa kutosha, sio rahisi kwenda kushiriki bila kuwa na uzoefu wa kutosha na kufanya vizuri.

“Lakini kwetu hili halitupi presha, bado tuna imani kubwa katika usajili ambao tumeufanya unaonyesha wazi kuwa tunataka kufika mbali, hatuna presha tunaamini katika mipango tuliyoiweka kuelekea mashindano hayo.”

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa