MUIGIZAJI na muongozaji wa filamu za Kibongo wa muda mrefu Jacob Stephen amesema kuwa Simba hii ya sasa inampa jeuri ya kuweza kuamini kuwa watani wao Yanga hawatakuwa na pakutokea.
JB alisema hajaiyona Simba ikicheza mechi nyingi kwa kipindi hiki igawa anaamini kwa majina na kwa mchezo ambao waliucheza dhidi ya St George unampa amani ya moyo na uwezo wa kutamba kuwa watani zao watakiona cha moto.
Akizungumzia mchezo huo JB alisema anajua kuwa hautakuwa mchezo rahisi kutokana na historia ya mechi za dabi na ubora wa Yanga na kile ambacho wamevuna msimu uliopita, ila anachoamini Simba hii ya sasa inakwenda kubadilisha kila kitu na inakwenda kuibuka na ushindi.
“Simba hii mpya inanipa jeuri na kusema kuwa timu yangu ni bora kuliko timu nyingine zote msimu huu, mimi mwenyewe inanitisha na sijui kwa upande wa wapinzani wetu watakuwa wapo kwenye hali gani.
“Kwahiyo Jumamosi tunakwenda kumfunga Yanga na kuchukua Ngao ya Jamii. Niamini maneno yangu haya, hawatufungi wale,” alisema.