Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limetangaza mpango wa kugawa jumla ya €31.5 milioni kwa vilabu vilivyowaruhusu wachezaji wao kushiriki michuano ya UEFA Nations League msimu wa 2024/25.
Malipo hayo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya UEFA Club Benefits Programme, mpango unaotokana na makubaliano ya UEFA na European Football Clubs (EFC), taasisi inayowakilisha zaidi ya vilabu 800 barani Ulaya.
UEFA imesema fedha hizo ni sehemu ya jumla ya €104 milioni zitakazotolewa kwa vilabu vilivyotoa wachezaji kwa ajili ya Nations League za 2024/25 na 2026/27, pamoja na mechi za kufuzu Euro 2028. “Mpango huu unanufaisha vilabu 611 kutoka katika vyama vyote wanachama wa UEFA, ikiwemo baadhi ya vilabu vya ngazi ya amateur,” UEFA ilisema katika taarifa yake.
RB Leipzig ya Ujerumani ndiyo klabu inayotarajiwa kupata kiasi kikubwa zaidi katika awamu hii, ikilipwa takribani €353,000 baada ya kuwaruhusu wachezaji wake 16 kushiriki mashindano hayo. Malipo hayo yanaonyesha namna UEFA inavyolenga kutambua mchango wa vilabu katika kutoa wachezaji kwa timu zao za taifa.
Katika fainali ya Nations League ya mwaka 2025, Ureno iliifunga Hispania kwa mikwaju ya penalti na kutwaa ubingwa. Wakati huo huo, msimu wa 2026/27 wa Nations League tayari umeanza, huku UEFA ikiendelea na utekelezaji wa mpango wake wa malipo kwa vilabu.


