Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba Zoran Manojlovic amefurahishwa na kuripoti mapema kwa mastaa watano wa kikosi hiko walioripoti kambini Misri siku ya Jumapili wakiwemo, Peter Banda na kiungo mpya wa kikosi hiko Moses Phiri.

Banda na Phiri ni miongoni mwa mastaa wa Simba ambao walichelewa kujiunga na timu hiyo nchini Misri kutokana na sababu mbalimbali, ambapo walilazimika kujiunga na timu siku ya Jumapili pamoja na wachezaji Henock Inonga, Nassoro Kapama na Taddeo Lwanga.

Simba waliwasili Misri kwa ajili ya kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya wa ligi 2022/23 Alhamisi ya wiki iliyopita na wanatarajia kurejea nchini Agosti 5, mwaka huu kwa ajili ya Tamasha la Simba litakalofanyika Agosti 8.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Tangu kuanza kwa kambi yetu hapa Misri siku ya Alhamisi jioni, naweza kusema tumekuwa na mafanikio makubwa sana kama kikosi ambapo tulianza na programu za mazoezi mepesi na yale ya utimamu wa mwili.

“Lakini kwa sasa tayari tumeanza mazoezi ya kimbinu ambapo kocha ameweka wazi kuwa anafurahishwa na maendeleo ya wachezaji wote katika utekelezaji wa programu zake, lakini ujio wa wachezaji wetu watano waliokuja siku ya Jumapili umemuongezea nguvu zaidi.”

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa