Hivi karibuni kumekuwa na mazingira ya kutunishiana misuli kati ya kocha wa Arsenal na maisha ya mchezaji Özil ambaye anakipiga katika kikosi hicho kwa kipindi kirefu kwa sasa huku akiwa ni mchezaji tegemezi sana ndani ya kikosi hicho cha miamba hao ambao kwa sasa wamekuwa hawana matokeo mazuri sana katika maendeleo ya kikosi chao kwenye michuano mbalimbali mikubwa.

Sakata hilo linaibua sura mpya kwa sasa kuona kwamba mchezaji huyo hapewi nafasi ya kuendelea kusalia kikosini hapo huku akikosa kabisa nafasi ya kucheza katika kikosi hicho kwa kuonekana kabisa kama anaandaliwa mazingira fulani ya kutimka kikosini hapo jambo ambalo yeye hayupo tayari kuachana na klabu yake hiyo ya kipindi kirefu katika ndoto zake za kucheza soka Uingereza.

Wakati hali hiyo ikiwa inaendelea mchezaji huyo ameamua kuweka ujumbe wake wenye tafsiri nzito katika mitandao yake ya kijamii yenye lengo la kumuonesha mwalimu huyo kwamba hajajiandaa kuondoka kikosini hapo leo wala kesho bali bado ana mengi ya kufanya ndani ya kikosi hicho.

Sio hilo tu, pia amejaribu kumwambia kwamba yupo kikosini hapo kwa sababu ya mapenzi yake na klabu hiyo. Maneno ya Özil yanasema ” Unapoishabikia klabu fulani hufanyi hivyo kwa sababu ya mataji, uwepo wa mchezaji fulani au historia, unafanya hivyo kwa sababu unajikuta tayari upo ndani ya familia ya aina hiyo; na unajikuta umefika pale ulipokuwa unatamani kupafikia siku nyingi.” Ameyanukuu maneno hayo kutoka kwa mkongwe wa klabu hiyo, Dennis Bergkamp.

Hii inaonesha kabisa kwamba mchezaji huyo hapendezwi kabisa na maamuzi ya mwalimu huyo kumkosesha nafasi za kucheza ndani ya kikosi hicho kutokana na sababu binafsi anazoziona kwa manufaa yake binafsi na sio ya klabu yake. Pamoja na hilo Özil anaendelea kuvuna mshahara wake mtamu wa £350,000 kwa wiki pamoja na kuwa hajapewa nafasi ya kucheza sana ndani ya utawala huo mpya.

Mara nyingi umekuwa ni mtindo wa makocha wengi kuwapoteza wachezaji wakubwa wanaoaminiwa na vikosi vya klabu zao pindi wanapopata nguvu za kuzinoa klabu hizo kwa wakati wao jambo ambalo kwa upande mwingine hufanya uongozi wa juu wa klabu husika kusimama kidedea na kulipinga suala hilo kama ni chuki binafsi.

Kwa wachezaji kama Özil bado wana kitu cha kuonesha katika vikosi vyao hivyo hakuna haja ya kuendelea kuzihama klabu walizopo na kuanza kupokea mishahara yenye makato makubwa ya hapa na pale ambayo kiuhalisia hayana maslahi yoyote. Au kuzihama klabu zao na kwenda kushusha uwezo wao katika klabu ambazo bado zinajijenga, kikubwa ni kuelewana na mwalimu arudi kikosini upya.

2 MAONI

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa