Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza rasmi kuwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga SC na Simba SC utapigwa Agosti 12, 2026, kuanzia saa 2:30 usiku katika Uwanja wa New Amani, Zanzibar. Taarifa hiyo imetolewa leo na TFF ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa msimu mpya wa soka nchini.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa soka, huku ukiwakutanisha mahasimu wa jadi wa Tanzania katika pambano la kuwania taji la kwanza la msimu wa 2026/2027. Ngao ya Jamii pia hutoa taswira ya utayari wa timu kuelekea mashindano ya ligi.
Hivyo pambano hilo litafungua rasmi pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2026/2027, ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maboresho yaliyofanywa na vilabu mbalimbali wakati wa dirisha la usajili.
Yanga na Simba zimekuwa zikitawala soka la Tanzania kwa miaka mingi, hivyo mchezo huo unatarajiwa kuvutia maelfu ya mashabiki watakaofika Uwanja wa New Amani pamoja na mamilioni ya watazamaji watakaofuatilia kupitia matangazo ya moja kwa moja.
Pamoja na hayo pambano hilo la kihistoria, ambalo litakuwa ishara rasmi ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, huku kila upande ukilenga kuanza kampeni zake kwa kutwaa Ngao ya Jamii.


