Benchi la ufundi la Coastal Union limefunguka kuwa kuwapoteza nyota wao Akpan na Sopu jambo hilo linawapa changamoto kubwa katika kutengeneza kikosi chao cha msimu ujao.
Akpan amejiunga na klabu ya Simba huku Sopu akitimkia kwenye klabu ya Azam, nyota hao walikuwa sehemu kubwa ya mafanikio ndani ya kikosi cha Coastal Union kwa msimu uliopita kiasi cha kuwashawishi mabosi wa timu hizo.
Akizungumzia hilo Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema kuwa tayari wameanza kutafuta mbadala wa wachezaji hao.
“Ni kweli tutakuwa na changamoto kidogo lakini kikubwa ni kuwa kama Kocha. Inabidi nitambue kwamba hilo litatokea tu kwani Akpan na Sopu hawakuzaliwa Coastal Union, sisi pia tuliwachukua sehemu hivyo kuondoka ni sehemu ya maisha yao, ila nawaombea sana Mungu awajalie huko wanapokwenda.
“Mimi kama mwalimu hiyo ni changamoto kwangu, na tunatafuta utaratibu mwingine wa kuhakikisha kwamba nitaziba yale mapengo na inshaallah yatazibika. Tupo kwenye zoezi la usajili ni sehemu ya kuhakikisha kwamba tunaziba hizo nafasi.”