UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa umepokea CV za makocha kutoka maeneo mbalimbali kwa makocha wenye uzoefu huku wazawa wakiwa ni wawili.
Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya Kaimu Kocha, Kali Ongala ambaye ameweka rekodi ya kuiongoza timu hiyo kwenye mechi 8 mfululizo za ligi kwa kushinda zote na kukomba pointi 24.
Hasheem Ibwe, Kaimu Ofisa Habari wa Azam FC alisema kuwa kwa sasa wataendelea kufanya kazi na Ongala kwa kuwa amekuwa na mwendelezo mzuri.
“Mtendaji Mkuu wa Azam FC, (Abdulkarim Amin) alimaliza kuhusu ujio wa kocha, Ongala amekuwa na mwendo mzuri na hilo tunajivunia hata msaidizi wake Agrey Morriss wamekuwa wakienda sawa na falsafa za wachezaji.
“Ukweli ni kwamba mpaka sasa kuna CV za makocha wenye uwezo zaidi ya sita na kati ya hizo, wawili ni wazawa hivyo mambo yakiwa sawa kila kitu kitakuwa wazi,” alisema Ibwe.
Ongala ambaye amebeba mikoba ya kuinoa Azam FC, Desemba 9,2022 alikiongoza kikosi hicho kushinda mabao 9-0 dhidi ya Malimao kwenye mchezo wa raundi ya Pili, Kombe la Shirikisho.