Yanga wanatakiwa kutumia Sh 150 mil ili wauvunje mkataba wa beki wao Mkongomani, Shaaban Djuma.
Yanga wamemuondoa katika mipango ya usajili ya timu hiyo, huku nafasi yake ikichukuliwa na Muivory Coast, Attohoula Yao.
Mkongomani huyo juzi hakutambulishwa katika kikosi cha Yanga cha msimu ujao kwenye Kilele cha Wiki ya Wananchi kilichofanyika juzi Jumamosi Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, beki huyo amekubali kuvunjiwa mkataba wa mwaka mmoja kwa sharti la kulipwa fedha.
Kocha huyo alisema kuwa, uongozi upo katika mazungumzo ya kuhakikisha wanauvunja mkataba wake huo alioubakisha. Aliongeza kuwa bado pande hizo mbili za uongozi wa Yanga na mchezaji wapo katika mazungumzo kwa ajili ya kufikia muafaka mzuri.
“Djuma hatakuwa sehemu ya wachezaji wetu katika msimu ujao, kwani tayari mchezaji mwingine tumempata aliyekuja kucheza nafasi yake. Hivi sasa tupo katika mazungumzo ya kuvunja mkataba wake huo wa mwaka mmoja ambao hivi karibuni tutatangaza kuachana naye rasmi.”
Hiyo ndio sababu ya hadi kushindwa kutangaza kuachana naye kama ilivyokuwa kwa Bangala Yannick ambao wote tupo nao katika mazungumzo ya kuvunja mikataba yao.
Alipotafutwa Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said kuzungumzia hilo simu yake iliita bila mafanikio ya kupokelewa.