KOCHA Mkuu wa Namungo, Cedric Kaze baada ya kuiongoza timu yake kwa mechi tano akikusanya pointi tatu na kupoteza kumi amesema mchezo dhidi ya Singida Big Stars umeshikilia hatma yake, hivyo anahitaji pointi tatu.
Namungo kwenye mechi tano ilizocheza imepoteza mbili na kutoka sare tatu ikianza na Kagera Sugar (1-1), Mashujaa (0-0), Yanga (1-0), KMC (1-1) na walikubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania.Akizungumzia mchezo huo watakaocheza wakiwa kwenye Uwanja wa Majaliwa ambao upo nyumbani kwao Ruangwa Lindi, Kaze ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga alisema anaingia kwenye mchezo dhidi ya Singida akiwa na uhitaji wa pointi tatu muhimu kwa lengo la kujihakikishia kibarua chake ndani ya timu hiyo.
Kaze alisema: “Natambua umuhimu wa pointi tatu kwenye mechi hii, natakiwa kujitengenezea CV nzuri ambayo itanibeba katika majukumu yangu nje ya Namungo ambayo nimekuwa nikipambania.
“Mchezo huu hautakuwa rahisi najua, kwa sababu hata Singida hawana wakati mzuri sana kama ambavyo tulivyo sisi. Lakini tunatakiwa kuwa na ubora zaidi ya tuliokuwa nao kwenye mechi zetu zilizopita.”
Namungo watavutana mashati na Singida kesho kutwa Jumamosi saa 1 usiku.