Klabu ya Yanga imetozwa faini ya Sh milioni 100 na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi baada ya wachezaji pamoja na benchi la ufundi kushindwa kutumia chumba rasmi cha kuvalia katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, na badala yake kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kamati hiyo, hatua ya Yanga imekiuka Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, huku adhabu hiyo ikitolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi. “Klabu ya Young Africans imetozwa faini ya Sh milioni 100 kwa kosa la kutotumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye uwanja wa mchezo kama inavyotakiwa na kanuni za ligi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Bila kusahau meridianbet ndio wakali wa ODDS KUBWA, Machaguo zaidi ya 1000 na kila kitu ukitakacho. Bashiri kijanja hapa
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imempeleka Rais wa Yanga, Hersi Said, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine, kwenye Kamati ya Maadili ya TFF ili kutoa maelezo kuhusu kile kilichoelezwa kuwa ni makosa ya kujirudia ya kukiuka kanuni zinazohusu matumizi ya vyumba rasmi vya kuvalia. “Viongozi hao wanatakiwa kutoa maelezo ya msingi kutokana na uvunjifu wa kanuni unaojirudia,” imesisitiza taarifa hiyo.
Kamati imebainisha kuwa hili si kosa la kwanza kwa Yanga, kwani mwezi Mei 2026 klabu hiyo iliwahi kupewa adhabu ya faini ya Sh milioni 30 kwa kosa kama hilo la kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja badala ya vyumba rasmi vya kuvalia vilivyotengwa kwa timu zinazoshiriki mchezo.
Hatua hiyo inaonyesha msimamo wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kuhakikisha klabu zote zinazingatia kanuni za mashindano, huku ikionya kuwa ukiukwaji wa taratibu za ligi utachukuliwa hatua kali bila kujali ukubwa au hadhi ya klabu husika.


