Mangungu Sio Mwisho wa Matatizo Simba

JUMA lililopita kulikuwa na hekaheka nyingi hususan kwa mashabiki wa Simba ambao baadhi yao walionekana kupaza sauti kuwa hawamtaki Mwenyekiti wao Murtaza Mangungu kuwa ndiyo chanzo cha matatizo yote klabuni kwao.

Hivi sasa mashabiki na wanachama wa Simba wamegawanyika makundi mawili wapo wanaoamini kuwa wachezaji ndiyo chanzo cha timu kutofanya vizuri na wapo ambao wanaamini kuwa uongozi ndiyo chanzo cha timu kuyumba.

Mashabiki wa Simba wanamjua mchawi wao lakini wanaogopa kumkabili na hapa ndipo tatizo lenyewe linaanzia.

Mchawi wa Simba ni katiba yao wenyewe kwa mujibu wa mzee wangu Ismail Rage amewahi kunukuliwa akisema kuwa katiba ya sasa ya Simba haiwapi mamlaka ya moja kwa moja wanachama ambao kikanuni kwenye upande wa hisa wana umiliki wa asilimia 51.

Upande wa mwekezaji ndiyo kila kitu na wote ni mashahidi kama mnakumbuka sababu ya aliyekuwa mwenyekiti wa Simba Swedi Nkwabi kujiuzulu nafasi yake ilitajwa kuwa ni mauzauza yaliyopo kati ya upande wa mwekezaji na upande wa wanachama.

Kiuhalisia Murtaza Mangungu hana nguvu yoyote mbele ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, bali anahesabika kama mjumbe tu hivyo kumbebebesha zigo la lawama ni kumuonea mashabiki na wanachama lieni na mabadiliko ya katiba yenu hapa ndipo mzizi wa tatizo ulipo na siyo kwa mzee Mangungu.

Mzee Mangungu hatujamuona kwenye matukio mengi makubwa yanayoihusisha Simba bali linapotokea ‘zingzong’ ndiyo mashabiki mnaibuka na kuanza kumnyooshea vidole jambo ambalo siyo sawa.

Kwenye mafanikio mwenyekiti wa klabu anatambulishwa Mo Dewji na wote ni mashahidi kwenye mechi ya ufunguzi wa AFL nani alimuona Mangungu jukwaa kuu akitambulishwa kama mwenyekiti wa Simba?

Kuhusu suala la timu kuwa na mwenendo usioridhisha hili lilikuwepo tangu msimu uliopita na tulishuhudia kauli tata nyingi kutoka kwa mwekezaji Mo Dewji kuhusu Simba nani alijitokeza hadharani kuhoji?

Simba inapofanya vizuri kimataifa moja kwa moja tunaona mwekezaji akijitokeza hadharani na kutamba lakini mambo yakienda kombo lawama zote kwa Mzee Mangungu.

Haya maandamano mliyopanga kuyafanya kuhusu kumtoa Mangungu madarakani badilisheni ajenda yenu muandamane kuhusu katiba mpya ya Simba ambayo imetoa mamlaka ya juu kwa upande wa mwekezaji na si upande wa wanachama wenye aslimia 51 za hisa kwenye klabu.

Shida kubwa mpira wetu umeingiliwa na siasa rahisi mimi naweza kuziita kuna maeneo kama taifa tukiyafanyia kazi ni wazi ubabaishaji kwenye mpira wetu utaondoka na hakutakuwa na hizi kelele za nani nafaa nani aondoke.

Ni kama mashabiki wa Simba wameamua kumtafuta mnyonge wao wa kumtwika zigo la lawama na wakaona Mzee Mangungu ndiyo mwepesi apewe msala huo.

Simba mchawi wa mafanikio yenu ni katiba mpya bila ya hivyo mtaendelea kuwakataa akina Mangungu kila kukicha. Karibu Temeke!

Acha ujumbe