Mwandishi na mchambuzi nguli wa soka nchini, Edo Kumwembe, amesema kuwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, anawaonea wivu YANGA.
Edo amesema: “Nadhani kuna tabia ambayo Mayele aliificha akiwa Yanga na sasa ameifichua. Kutaka kuonekana mkubwa na mfalme.“Bahati mbaya inamuumiza pia kwamba Yanga wanasonga mbele bila ya yeye. Huwa inatokea unapoachana na mpenzi wako. Hautaki yamtokee mema mbele ya safari.
“Lakini kuna uwezekano mkubwa Mayele anaumwa ugonjwa wa kupenda nyumbani (home sickness). Tayari Tanzania kulishakuwa nyumbani kwake na aina ya maisha ya Tanzania yalimuingia kwelikweli.
“Maisha ya uwanjani, mitaani na mitandaoni. Tanzania bado haijamtoka. Bado ipo akilini mwake. Mwili upo Misri, lakini akili ipo Tanzania.
“Inawatokea wageni wengi waliowahi kuishi Tanzania. Sio tu wanasoka kama kina Bernard Morrison ambao tunaona kila siku wanazurura Dar es salaam ingawa wanacheza soka la kulipwa Morocco, lakini pia kwa wageni wengine.
“Hata kuna mabalozi wa nchi za nje hawaishi kurudi kutembea Tanzania baada ya muda wao kwisha.“Mayele sio maarufu DR Congo kuliko Tanzania. Hii ina maana simu yake yote ina habari za Tanzania na yeye binafsi angependa kuwa sehemu ya habari hizo. Haishangazi kuona haachi kuzusha jambo hili na lile.
“Inawezekana kweli alipitia anachopitia lakini inawezekana pia imewatokea wachezaji wengi waliopita Simba na Yanga, hata hivyo hawana habari ya kulalamika kupitia simu zao wala redioni.“ Edo Kumwembe.