BAADA ya kutangazwa kuachwa na klabu ya Yanga Princess kocha Edna Lema maarufu kwa jina la ‘Mourinho’ ametoa neno la shukrani kwa Uongozi wa timu hiyo pamoja na mashabiki na kuomba kusamehewa kama kuna sehemu alikosea.
Kupitia mtandao wake wa Instagram Edna (Mourinho) aliandika ujumbe huu:
“Kwanza nianze kwa kushukuru viongozi wa Yanga kwa ushirikiano walionipa kwa muda niliokuwa hapa, niwashukuru pia wachezaji wangu kwa mapenzi mliyokuwa nayo kwangu kwa ushirikiano mlionipa, niwashukuru mashabiki kwa sapoti yao kubwa kwangu na kwa timu kwa ujumla nadiliki kusema Yanga wamenikuza na kunifanya kuwa mkubwa pengine hata ukubwa nisio stahili kwa sababu ni klabu kubwa.
“Najua kila shabiki anaitakia mema hii timu na anatamani ipate mafanikio, nilijitahidi kufanya kile kilichokuwa ndani ya uwezo wangu lakini kwa sasa inatosha kwa hapa nilipofika mpaka wakati mwingine, pengine hii timu inahitaji maisha mengine yasiyokuwa na Edna Lema (Mourinho) ili iweze kufanikiwa najua pia kuna machache mazuri nimeyafanya mpaka hii timu kufikia hapa japo sikufikia malengo
“Hatuwezi kuwa maadui kwa sababu mimi sio sehemu ya Yanga bado mtabaki kuwa familia yangu mimi na viongozi pamoja na mashabiki, niwashukuru tena na tena kwa mapenzi yenu kwangu, najua kuna wanaonipenda sana lakini timu kwanza mtu baadae.
“Kama kuna tulipokoseana tusamehane maisha mengine yaendelee. Daima mbele nyuma mwiko”
Mnamo Juni mwaka jana 2021, Edna Lema ‘Mourinho‘ alishindwa kufikia makubaliano na klabu ya Yanga Princess na hivyo Sekretarieti ya klabu hiyo ikaamua kuachana nae kabla ya kurejeshwa tena klabuni hapo Disemba 2021.