Mlinda mlango namba moja wa Simba, Mousa Camara ameandika rekodi yake ya kuwa namba moja kwa makipa wenye hati safi ndani ya uwanja akiwa ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Camara ndani ya ligi ni mechi 18 kacheza akikomba dakika 1,620 akiwa ni miongoni mwa wachezaji waliokomba dakika nyingi ndani ya uwanja kwenye mechi za ushindani.
Mousa Camara kafungwa mabao sita ndani ya ligi namba nne kwa ubora ilikuwa mabao mawili dhidi ya Coastal Union, mawili dhidi ya Kagera Sugar, bao moja dhidi ya Yanga na bao moja dhidi ya Fountain Gate.
Ipo wazi kwamba alianza kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi ambapo Mousa Camara alionekana kufanya makosa katika kuokoa mpira wa faulo iliyopigwa na kiungo Clatous Chama uliporudi ndani ya uwanja ukakutana na Maxi Nzengeli ambaye alipiga krosi kuelekea langoni ikakutana na Kapombe Shomari ambaye aliokoa hatari hiyo.
Wakati Kapombe akimalizia kuokoa hatari beki wa Simba, Kelvin Kijili aliyekuwa karibu na lango la Simba mpira ule ukamgonga na kuzama mazima nyavuni, Simba ikayeyusha pointi tatu mazima.
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra amekaa langoni kwenye mechi 12 akikomba dakika 1,080 ni mabao matano kafungwa kipa huyo ndani ya msimu wa 2024/25 akiwa na hati safi 9.
Ni Machi 8 2025 inatarajiwa kuchezwa Kariakoo Dabi kwa wababe hao kukutana ndani ya uwanja katika msako wa pointi tatu muhimu.