ACHANA na nafasi yake ya kiungo anayocheza, Muivory Coast, Pacome Zouzoua, lakini Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe amesema kuwa ipo siku staa huyo atachezeshwa namba 9 katika mechi na kocha wake, Miguel Gamondi kutokana kiwango bora alichonacho.
Katika mchezo wa juzi uliochezwa juzi dhidi ya KMC, kiungo huyo alionyesha ubora na umahili wa kupiga pasi za mwisho kwa wachezaji wenzake huku akifunga bao moja katika ushindi wa mabao 5-0.Kiungo huyo, huo ndio mchezo wake wa kwanza kuucheza kwa dakika 90, tangu ajiunge na Yanga katika msimu huu akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Kamwe alisema kuwa ubora wa Yanga wa msimu huu ni kama ya Timu ya Taifa ya Hispania ya mwaka 2010 yenye viungo wengi mafundi wenye uwezo wa kufunga na kutengenezeana nafasi za kufunga mabao.
Kamwe alisema kuwa ipo siku kocha wao Gamondi, atampanga Pacome nafasi ya ushambuliaji namba 9, kama Cesc Fabregas akiwa anaichezea Hispania 2010 ambaye yeye ni kiungo halisia mwenye uwezo wa kuchezesha timu na kufunga ndani ya wakati mmoja.
Aliongeza kuwa kiungo wao amelithibitisha hilo katika mchezo dhidi ya KMC ambaye alifunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao, kama wachezaji wenzake wangezitumia vema, basi wangepata ushindi wa mabao zaidi ya hayo 5-0.
“Nilitukanwa sana wakati msimu unakaribia kuanza wa msimu huu, ni baada ya kutamka kuwa Yanga ya msimu huu ni bora zaidi ya uliopita, wengi hawakuamini katika hilo, lakini sasa wameanza kukubali nilichokiongea.
“Nilipata jeuri ya kuongea hayo, ni baada ya kuangalia mazoezi ya timu kambini Avic Town, niwaambie mashabiki wa Yanga kuwa huyu Pacome ipo siku atapangwa kucheza namba 9, hapo ndio utakapojua ubora wake, licha ya nafasi yake kuwa kiungo.“Yanga hii ni kama Timu ya taifa ya Hispania ya mwaka, 2010 ambayo ilikuwa ikimtumia Fabregas kucheza namba 9, ndio Pacome atakapochezesha nafasi hiyo na kuthibitisha ubora wake wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao,” alisema Kamwe.