Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema kuwa watani zao, Klabu ya Yanga wanapaswa kupongezwa kutokana na soka safi wanalocheza hivi sasa na kupata matokeo mazuri kwenye michuano ya Kimataifa lakini wasibweteke.
Rage amesema hayo kufuatia matokeo mazuri waliyopata Yanga juzi, Februari 24, 2024 kwa kuifunga CR Belouizdad bao 4-0 na kutinga hatua ya robo fainali ya CAFCL wakiwa na mchezo mmoja mkononi, na kuvunja rekodi yao ya miaka zaidi ya 52 iliyopita kufika hatua hiyo.“Ninawaona kabisa Yanga wakivuka robo fainali, lakini wasibweteke na ushindi walioupata juzi. Hii ndiyo madhaifu ya timu zetu za Tanzania, wakishinda mara moja wanajisahau sana. Mimi (Simba SC) nimeshampiga Horoya hapa bao 7 nikajisahau kidogo nikatolewa.
“Kama waliweza kuingia fainali Kombe la CAFCC wanaweza kuingia fainali pia CAFCL. Hata ukiangali timu nyingi zilizokuwa zinatawala AFCON ziliondolewa mapema, timu ambazo hazikupewa nafasi ndizo zilifanya vizuri kwa sababu walijiamini.“Yanga wakienda kwa kujiamini wanaweza kumfunga Al AHly pale pale kwao, kama Simba waliweza kwa nini Yanga washindwe?,” amesema mzee Rage