IKIWA imebaki siku mbili kabla ya Simba hawajafunga hesabu za kuvuka kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapocheza na Power Dynamo kesho kutwa Jumapili, bosi wa klabu hiyo ametoa kauli nzito.
Simba watacheza Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi saa 10 jioni, wakiwa na hesabu mbili tu muhimu, kushinda au kutoa sare ili wavuke. Sasa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amesema Chamazi inakwenda kubadilishwa rangi na kuwa nyeupe na nyekundu.Ahmed amesema, wanataka hadi kufikia saa 6 mchana, uwanja huo uwe umejaa mashabiki ambao watakuwa wamevaa jezi zao nyeupe kwa nyekundu, kisha watafanya vurugu za kushangilia kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho wa mchezo huo.
Ahmed Alisema: “.Kikosi cha Simba SC, muda huu kinafanya mazoezi katika uwanja wa Azam Complex kujiandaa na mchezo dhidi ya Power Dynamos ya Zambia utakaopigwa Jumapili hii.
“Katika uwanja wa Azam Complex, kunakwenda kubadilika siku hiyo, kwanza tumeumisi ule Uwanja na ni sehemu ambayo Simba uwa tunafanyaga makubwa kila tukicheza pale. Hivyo tunakwenda kuubadilisha muonekano.“Rangi za jezi na nyekundu ndiyo zitaupamba, hadi kufikia saa 6 utakuwa umejaa na haijawahi kutokea hiyo kitu. Kisha tutapiga makelele mwazo mwisho, huku tukienda makundi kwa madoido,” alisema Ahmed.
Simba kwa sasa inafanya mazoezi Azam Complex kwa ajili ya wachezaji wake kuuzoea uwanja kabla ya mchezo wa marejeano ambao awali walitoka sare ya mabao 2-2 pale Ndola, Levy Mwanawasa, nchini Zambia.