Mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga limeanza kuvutia, baada ya hesabu kubadilika na kuwa sasa kila mmoja ashinde tu mechi zake, hali iliyokuja baada ya Simba Chini ya Barker kushinda mbele ya Coastal Union na kukaa kwenye msimamo wa ligi kwa muda kidogo kwa tofauti ya alama moja.

Simba walifikisha pointi 55, wakati Yanga walikuwa na 54, lakini walikuwa bado hawajacheza mchezo wao dhidi ya Singida Black Stars na waliposhinda wakarudi kwenye kilele cha msimamo wakiwa na tofauti ya alama 2 dhidi ya Mnyama Simba.
Hali hiyo ya ushindani kuongezeka imemuibua Kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, ambaye amesema kikosi chake hakitaki kujihusisha sana na hesabu za wapinzani wao, bali kimejikita katika kuhakikisha kinashinda kila mchezo unaokijia bila kuyumbishwa na presha ya msimamo wa ligi.
Barker amesisitiza kuwa falsafa yake ndani ya kikosi hicho ni kujenga utamaduni wa ushindi wa mfululizo, akibainisha kuwa kila mchezo una uzito sawa bila kujali kama ni dhidi ya timu ya juu au ya chini kwenye jedwali.
Ameongeza kuwa hali ya Simba kucheza baadhi ya mechi kabla ya Yanga ni tofauti na ilivyozoeleka katika misimu mingine, lakini hilo halibadili malengo yao kwani wanachokilenga ni kukusanya pointi zote muhimu bila kujali ratiba ya wapinzani.



