BAKARI Mwamnyeto nahodha wa Yanga ameweka wazi kuwa moja ya sababu kubwa iliyofanya wakakosa ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania ni sehemu ya kuchezea kutokuwa rafiki.
Mchezo wa mzunguko wa pili kati ya JKT Tanzania na Yanga ulichezwa Aprili 24 2024 ambapo awali ulitarajiwa kuchezwa Aprili 23 lakini uliahirishwa kutokana na hali ya hewa ya mvua iliyofanya mpira kushindwa kudunda eneo la kucheza.Baada ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo ubao ulisoma JKT Tanzania 0-0 Yanga timu zote mbili ziligawana pointi mojamoja baada ya mchezo kukamilika.
Mwamnyeto ameweka wazi kuwa ulikuwa ni mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa hawakuwa na namna kwa kuwa waliambiwa wacheze hivyo walitimiza majukumu yao kwa umakini.
Mara baada ya mchezo kupitia mahojiano na Azam TV, nahodha huyo alibainisha hayo kuhusu mchezo wao.
“Kikubwa ilikuwa sehemu ya kuchezea haikuwa rafiki kwetu, uwanja ulijaa matope kwenye baadhi ya sehemu hivyo kutupa tabu kucheza lakini tunamshukuru Mungu tumepata pointi moja.“Malengo ilikuwa ni kupata pointi tatu muhimu ila kwa hii pointi moja sio mbaya licha ya kwamba tumepoteza pointi mbili kwenye mchezo wetu,”.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kusalia namba moja kwenye msimamo na pointi 59 baada ya kucheza mechi 23 huku JKT Tanzania ikiwa na pointi 23 kibindoni.