YAO KOUASSI AJIPATA YANGA

Yanga SC iko zake kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kukusanya alama 40 katika mechi 15 ilizocheza ikiwa katika harakati za kutetea taji la Ligi Kuu Bara, huku beki wake Muivory Coast, Kouassi Attohoula Yao (27) akianza kunusa ufalme mapema.

Yao , beki wa kulia wa Yanga kabla ya mechi za juzi alikuwa kinara wa kutoa pasi za magoli ‘asisti’ akifanya hivyo mara sita sawa na winga wa Azam FC, Kipre Junior.

Huenda msimu huu ukawa wa kifalme kwa Yao kutokana na rekodi za asisti zilivyo katika misimu mitatu iliyopita kwa wachezaji wanaocheza eneo la ulinzi, yaani mabeki.YANGAKatika misimu minne iliyopita kwenye Ligi Kuu Bara ni beki mmoja tu, Shomari Kapombe aliyekuwa akimiliki ufalme huo kwani ametoa asisti kuanzia tatu na kuendelea kwenye kila msimu.

Hata hivyo, Kapombe ndiye beki aliyetoa asisti nyingi zaidi kwenye msimu mmoja. Ilikuwa msimu uliopita wa 2022/2023 alipotoa asisti nane.

Katika msimu huo, Kiungo Mzambia wa Simba, Clatous Chama ndiye alikuwa kinara wa Asisti akitoa 14 akifuatiwa na Saidi Ntibanzonkiza aliyetoa 10.

Kapombe alikuwa beki mwenye asisti nyingi akiwa nazo nane akifuatiwa na Mohamed Hussein wa Simba aliyefanya hivyo mara sita.

Tayari Yao, amemfikia Hussein na sasa anaitafuta rekodi ya Kapombe ikiwa amebakiza mechi 15 za ligi jambo ambalo akiendelea na kiwango chake cha sasa ana nafasi kubwa ya kuzifikia na hata kuzidi na kujitengenezea ufalme wake.

Ukichukua asisti za Yao kwa msimu huu ukazipeleka msimu wa 2021/2022, basi angekuwa kinara wa kupiga pasi za mwisho katika msimu huo.

2021/2022 ulikuwa msimu mgumu kwa wakali wa Asisti kwani walioongoza walikuwa nazo sita pekee. Ni Abdulhaman Mussa wakati huo akiwa Ruvu Shooting na Reliants Lusajo aliyekuwa Namungo. Waliibuka vinara baada ya kila mmoja kupiga asisti sita. Kwa sasa wawili hao wote wako Mashujaa FC.YANGADjuma Shaban ndiye aliongoza kwa mabeki waliotoa asisti nyingi msimu huo akiwa Yanga akitoa tano ambazo tayari Yao amezipita.

Beki mwingine aliyeingia kwenye orodha hiyo alikuwa Aboubakar Ngalema wa Dodoma Jiji aliyetoa nne huku Kapombe akiingia pia baada ya kumaliza msimu na asisti tatu sawa na Lusajo Mwaikenda (Azam) na Bruce Kangwa aliyeondoka.

Acha ujumbe