Aibu ya Soka la Afrika!

Soka letu la Kiafrika linaonekana kuwa na safari ndefu sana ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho makubwa sana kuanzia suala la maamuzi na uwekezaji mkubwa. Limekuwa ni soka lililotawaliwa na vitimbwi vya kila aina huku wengine wakiumizwa kwa maamuzi magumu na yasiyo sahihi yanayojitokeza.

Ugumu wa soka letu huonekana kuwa na tatizo kubwa ambalo linaonekana kama ni upangaji wa matokeo nje ya uwanja. Wengi husema kwamba mechi nyingi kubwa za Afrika huchezwa kwanza nje ya uwanja na ndipo uwanjani kwa kuendana na maamuzi ambayo sio sahihi kwa timu ya upande fulani.

Tamthiliya hiyo ilijitokeza kwenye mechi ya fainali ya klabu bingwa Afrika, CAF kati ya Esperance de Tunis na Wydad Casablanca. Ndani ya mechi hiyo kulitawaliwa na maamuzi yenye utata wa kila aina ambao kwa upande fulani ulichangia kuvunjika kwa ustaarabu ndani ya mechi na hata kufanya wengine kufanya vitu ambavyo havikuwa vya kiungwana.

Esperance de Tunis walisimikwa mabingwa wa kombe hilo baada ya upande wa pili wa mshindani wao kugomea mechi wakimtaka muamuzi kuangalia kwenye kisaidizi cha video (VAR) baada ya goli lao kuzuiliwa ikisemekana waliotea wakati wakifunga goli hilo na wao hawakuweza kukubaliana na maamuzi hayo.

Mikwaruzano hiyo iliibuka dakika ya 58 ya mechi hiyo baada ya muamuzi kuzuia jitihada zilizofanywa na kiungo hatari wa Wydad, Walid El Karti ambaye aliipatia timu yake hiyo ushindi kwenye dakika hizo lakini muamuzi, hata baada ya shinikizo la kutumia VAR, aligoma kwa kukomalia maamuzi yake ya awali.

Muamuzi huyo wa Gambia, Bakari Gassama alionekana dhahiri kuegemea upande fulani kimaamuzi ndani ya mechi hiyo baada ya kuwa na maamuzi yasiyokuwa na usawa kabisa ndani ya mechi hiyo. Halikuwa jambo zuri kwa kuonekana wazi kwamba amedhamiria nani aondoke kifua mbele ndani ya mechi hiyo.

Hilo liliweza pia kutokea katika mechi ya kwanza kati ya wawili hao ambapo maamuzi yalikuwa mabovu sana. Hii sio picha nzuri kwa soka ambalo linaangaliwa kukua hata kiuwekezaji lakini kwa uchafuzi huu bado itabaki kuwa historia tu.

Hili sio tukio la kwanza inakumbukwa mwaka 2018 pale Gor Mahia walipokuwa wakishiriki huko Tunisia walifanyiwa figisu za aina hii hadi kuwapelekea kutamkiwa maneno yasiyo ya kiuungwana. Safari yetu bado ni ndefu sana hakika!

2 Komentara

    God bless Africa 🙏❤️❤️❤️

    Jibu

    Asanteh kwa taarifa meridianbet

    Jibu

Acha ujumbe