Alessandro Bastoni amekuwa na mwanzo mgumu wa mwaka 2026, huku FC Barcelona wakiwa tayari kujaribu kumsajili beki huyo wa Inter Milan majira haya ya joto.

Bastoni ameambiwa huenda akalazimika kuondoka Italia kufuatia kampeni mbaya ya kufuzu Kombe la Dunia ya Italy.
Washindi wa FIFA World Cup 2006 walikosa nafasi ya kushiriki mashindano hayo baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Bosnia and Herzegovina katikati ya wiki.
Bastoni alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika mchezo huo baada ya kumchezea rafu ya mwisho Amar Memic, muda mfupi baada ya Moise Kean kuipa Italia uongozi chini ya Gennaro Gattuso.
Hii inaongeza kwenye mwanzo mbaya wa mwaka kwa beki huyo wa miaka 26, ambaye pia alikosolewa kwa tukio la kujiangusha katika Derby d’Italia lililosababisha beki wa Juventus, Pierre Kalulu, kutolewa nje.

Bastoni alionekana kushangilia uamuzi huo, jambo lililozua ukosoaji mkubwa. Aliyezomewa wakati wa ushindi wa Inter wa 2-0 dhidi ya Lecce, huku familia yake ikipokea vitisho vya kifo kufuatia tukio hilo kwenye ushindi wa 3-2 dhidi ya Juventus.
Sasa, gwiji wa zamani wa Inter na Italia, Giuseppe Bergomi, amesema kuwa Bastoni anaweza kulazimika kuondoka Italia ili kuokoa taaluma yake.
“Tumemfanyia nini huyu kijana. Ni rafiki yangu, namuona mara kwa mara, nampenda sana. Makosa hutokea, lakini ameishiwa na uvumilivu baada ya yote aliyopitia kwa zaidi ya mwezi mmoja. Sasa kwa manufaa yake mwenyewe, atalazimika kuondoka Italia, na tunapoteza kipaji kikubwa, mmoja wa mabeki bora wa kisasa. Ana mazuri na mapungufu yake”. Alisema Bergomi



