Mchezaji wa Ajax Edson Alvarez amefunguka kuhusu pigo lake la kukosa kuhama kutoka Ajax kwenda Chelsea, lakini kiungo huyo wa kati wa Mexico anatarajia klabu nyingine kubwa Ulaya kuja kumnunua dirisha la Januari.
Alvarez ambaye ana umri wa miaka 25 anatazamiwa kuwa mtu muhimu kwa nchi yake kwenye Kombe la Dunia linalotarajiwa kupigwa Qatar 2022, ambapo atakuwa na nafasi nyingine ya kuvivutia vilabu vikubwa Ulaya.
Mchezaji huyo wa zamani wa Club America ilisemekana kuwa alikuwa chini ya ofa ya Euro milioni 50 kutoka kwa Chelsea katika dirisha lililopita la usajili, jambo ambalo Ajax walikataa kumuachia kiungo huyo huku mchezaji huyo akisema kuwa amesikitishwa na kukosa dili hilo.
Alvarez na timu yake ndiyo vinara wa ligi hiyo ya Eredivisie , hata baada ya kuwapoteza baadhi ya wachezaji wao kama Antony na kocha wao mkuu Erik ten Hag kwenda Manchester United, timu bado inafanya vizuri. Edson anasema kuwa;
“Bila shaka kulikuwa na nia kutoka kwa Chelsea. Hakuna aliyetarajia kwamba wangetoa ofa nyingine,” Alvarez alisema. “Ajax hawakuweza kwenda popote. Hawakuweza kufanya lolote zaidi. Hawakuwa na mchezaji katika nafasi yangu.”
Mchezaji huyo amekuwa akicheza kwa juhudi zote na kujitoa kwa timu hiyo huku akijua kwamba ipo siku atakuwa mchezaji bora na kwenda kutafuta changamoto nyingine kwa timu kubwa ambazo ataenda.
Hakuishia hapo tuu, aliongeza kwa kusema kuwa anafahamu kila kitu kinabadilika na siku zote amekuwa akijifikiria kuwa yupo hapo sababu ya kupenda soka lakini pia ni kwaajili ya familia yake.
Na pia anapata motisha kubwa kwakuwa vilabu vikubwa vinafuatilia mechi zake, vitendo vyake, lakini amesikitishwa sana kutokwenda Chelsea na ana uhakika hivi karibuni klabu kubwa itakuja kwaajili yake.