KATIKA mabao 38 ambayo safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga kinara wa utupiaji ni Leonel Ateba ambaye katupia mabao 8 msimu wa 2024/25.
Ni mabao manne amefunga kwa penalti ikiwa inamanisha kuwa hajawa imara katika kumalizia nafasi ambazo anatengenezewa ndani ya uwanja hasa krosi.
Katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Ateba alikosa nafasi zaidi ya tano za wazi akiwa ndani ya 18 ikiwa ni pamoja na ile aliyobaki yeye na lango kazi yake kuchagua upande kujaza mpira kambani.
Kwenye mchezo huo uliochezwa Februari 11 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC ulisoma Simba 3-0 Prisons, mabao ya Jean Ahoua ambaye naye anafikisha mabao 8, Mpanzu na Ladack Chasambi likiwa ni bao lake la kwanza ndani ya Simba kufunga kwa upande wa Simba ukiweka kando lile la kujifunga dhidi ya Fountain Gate.
Kwenye mchezo dhidi ya Prisons Ateba alipigiwa krosi matata kutoka kwa Zimbwe Jr dakika ya 43 ilimkuta akiwa katika nafasi nzuri ni baada ya kipa Sebusebu kupishana na mpira huo.
Mpango kazi wake akitumia mguu wa kulia haukuwa na bahati nzuri kwa kuwa pigo lake hilo lilikwenda nje kidogo ya lango.
Ukiweka kando hilo alikosa nafasi nyingine dakika ya 15, 35, 62 na 70 ni pasi moja ya bao alitoa dakika ya 44 alimpa Ellie Mpanzu ambaye alifungua akaunti yake ya mabao ndani ya ligi msimu wa 2024/25 akiwa na uzi wa Simba.