Klabu ya Bayern Munich hii leo itamkaribisha Bayer Leverkusen katika mchezo wa raundi ya nane wa Bundesliga baada ya mapumziko ya Kimataifa kumalizika na sasa ligi mbalimbali kurejea kuanzia hii leo.
Bayern walianza vizuri mechi takribani tatu, lakini hatimaye mambo yakaanza kuwa mabaya ambapo walifululiza kupata sare tatu na mchezo wa mwisho walipoteza kwa bao 1-0 wakiwa ugenini dhidi ya Augsburg.
Timu hiyo ambayo ipo chini ya kocha mkuu Julian Nagelsman inatarajiwa kuingia dimbani hii leo kutafuta alama tatu ambazo wamezikosa ndani ya mechi nne huku kukiwa na taarifa nyingi zikisema kuwa inawezekana kibarua cha Nagelsman kuwa hatarini.
Timu hiyo imekuwa ikisuasua kwani baada ya aliyekuwa mshambuliaji wao Roberto Lewandowski kutimkia Barcelona hawajasajili namba 9 kabisa na sasa shida inaonekana kwenye kupata magoli kitu ambacho hawajawahi kukabiliana nacho.