Moises Caicedo amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na Brighton and Hove Albion baada ya uhamisho wake kushindwa kukamilika kwenda Arsenal.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21 alihusishwa pakubwa na kuondoka kwenye Uwanja wa Amex wakati wa dirisha la usajili la Januari, akieleza hadharani nia yake ya kuhamia vinara wa ligi Arsenal.
Kikosi cha Mikel Arteta kiliripotiwa kutoa ofa ya hadi pauni milioni 70 na kukataliwa na Brighton na kulikuwa na matarajio kwamba Gunners wangerejea kwa Caicedo mwishoni mwa msimu.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa Kimataifa wa Ecuador sasa ametoa ahadi yake kwa Seagulls kwa mkataba mpya utakaodumu hadi 2027, na chaguo la klabu kwa mwaka zaidi.
Kocha mkuu wa Brighton Roberto de Zerbi amesema; “Hizi ni habari nzuri kwa klabu, mashabiki wetu, kwangu na muhimu zaidi kwa Moises. Itatufanya tuwe na nguvu zaidi tunaposonga mbele kuelekea malengo yetu uwanjani.”
Caicedo alijiunga na Brighton mnamo Februari 2021 kutoka Independiente del Valle, kisha akatumia nusu ya kwanza ya msimu uliofuata kwa mkopo na Beerschot ya Ubelgiji.
Mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza ilikuja katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Arsenal mnamo Aprili 2022, huku Caicedo akihifadhi nafasi yake kwa kipindi kilichosalia cha msimu na kucheza sehemu muhimu msimu huu.
Brighton wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kuu, pointi nne nyuma ya Liverpool iliyo nafasi ya sita na wakiwa na michezo mkononi juu ya washindani wao wa karibu.