MLINDA mlango namba moja wa kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, Moussa Camara amesema kuwa bado kazi inaendelea kimataifa watapambana kufanya kweli na kupata matokeo katika mechi zijazo.
Ipo wazi kwamba kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos, uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Novemba 27 2024 Camara aliokoa penati dakika ya 48 mwisho Simba ilishinda kwa bao 1-0.
Ni mkandaji Kibu Denis alisababisha penati hiyo kwenye harakati za kuokoa hatari hasa kipindi cha pili ambapo wapinzani wao kutoka Angola walikuwa wakisaka kupata bao kwenye mchezo huo.
Kipa huyo amebainisha kuwa kwenye mchezo uliopita walipata ushindi jambo ambalo ni kubwa na kipindi cha pili wapinzani wao walikuwa wakitafuta kuwafunga.
“Kwenye mchezo wetu kipindi cha kwanza tulipata bao la kuongoza na kipindi cha pili wapinzani wetu walikuja kwa kasi wakiwa na lengo la kupata bao mwisho tulilinda ushindi wetu na haikuwa rahisi hivyo kazi bado inaendelea. Alisema Camara