Ripoti kutoka Italia zinazidi kuonyesha kuwa Como ipo karibu kufikia makubaliano na Chelsea ya kumsajili beki Trevoh Chalobah, baada ya kukubali kulipa ada ya euro milioni 30 ambayo Chelsea ilikuwa ikiihitaji kama kiwango cha kudumu cha uhamisho wake.

Pia alikuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa na Inter Milan, huku kukiwa na taarifa kuhusu makubaliano ya kutoshambuliana kati ya klabu hizo mbili za Serie A katika mbio za kumsajili.
Hata hivyo, baada ya Inter kujiondoa katika harakati za kumnasa na badala yake kuelekeza nguvu kwa John Stones na Cristian Romero, nafasi ikafunguka kwa Como kurejea kwenye mazungumzo ya kumsajili.
Kwa mujibu wa Fabrizio Romano na mtaalamu wa masuala ya uhamisho wa Calciomercato, Daniele Longo, Como sasa ipo karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kufikia makubaliano na Chelsea.
Chelsea ilikuwa imeweka bei ya euro milioni 30 za ada ya moja kwa moja pamoja na euro milioni 5 za nyongeza (add-ons). Hata hivyo, hadi sasa Como ilikuwa imesita kukubali kiasi hicho kama sehemu ya uhakika ya malipo ya dili hilo.

Inaonekana sasa wanaelekea kukaribia kufikia kiwango hicho kwa ajili ya beki huyo wa kati wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 27.


