Erling Haaland, Mkaka Mwenye ‘Future'

Msemo ‘mkaka mwenye future’ hutumiwa sana na akina dada wakiwapamba aina ya wanaume wanaowapenda au ambao wangependelea kuanzisha mahusiano nao. Utawasikia wakisema “sitaki sharobaro mimi,  nataka mkaka mwenye future”, wakimaanisha kuwa wanataka mwanaume ambaye kesho yake inaeleweka. Sikubaliani nao, japo pia siwapingi kuwa huyo wanaemuita sharobaro hana ‘future’. Mambo yao tuwaachie wenyewe. Leo msemo huo utaleta maana hapa,

Unamfahamu Erling Braut Håland? Kama wewe ni mtu wa mpira bila shaka umejibu “ndiyo”.  Namzungumzia yule dogo aliyewalaza Genk ya Samatta na wenzie na viatu usiku wa September 16 2019 katika mashindano ya klabu bingwa ya Ulaya kwa kuwatundika magoli matatu ‘hat trick’ peke yake katika ushindi wa RB Salzburg wa magoli 6-2. Hakubahatisha, dogo ni moto wa kuotea mbali hata kabla ya hapo.

Haaland ameshafanya makubwa sana tu tangu akiwa kikosi cha vijana cha Bryne Fk , yani Bryne 2. Dogo alitundika kambani magoli 18 katika michezo 14 tu aliyocheza. Hapo hata kama wewe ndio ungekua kocha wa kikosi cha wakubwa unaachaje kumjumuisha hapo? Kocha akawa hana jinsi, pamoja na umri wake kuwa mdogo ikabidi apandishwe kikosi cha wakubwa.

Hapo akavutia macho ya aliyekua mwalimu wa kikosi cha Molde FK, Ole Gunnar Solskjaer. Hapo pia dogo hakufanya masihara, inaonekana kama ana undugu na goli huku akiwa na uadui na walinda mlango kwani katika mechi yake ya kwanza tu akiwa na Molde alitupia kambani. Msimu wa pili tu akiwa na Molde yani 2018 alibeba tuzo ya mfungaji bora wa klabu akiwa na magoli 16 katika michezo 30 aliyocheza. Unaona sasa? Haaland na nyavu za magoli damdam!

Redbull Salzburg walikiona kile kilichopo ndani ya Haaland, ikawabidi kuvunja kibubu wapate saini ya kinda huyu. Hawakukosea, macho yao hayakuwadanganya. Msimu wake wa kwanza tu akiwa na RB Salzburg alifanikiwa kutupia kambani magoli 16 katika michezo 14 aliyoanza. Undugu wake na nyavu uliendelea kujidhihirisha hapo.

Dogo ni kama alikua anatuma salamu kwa vilabu vikubwa vya ulaya kuwa vimuone. Nao ni kama vile walidharau salamu hizo kwani walimuacha aendelee kubaki palepale Salzburg. Dogo akaona sasa wasimtanie, akawapelekea habari palepale kwenye mashindano yao. Mashindano ya vigogo ‘UEFA’ Champions League. Dogo aliingia kambani mara 8 katika mechi sita za hatua ya makundi alizocheza katika klabu ya mabingwa. Kisha akakaa pembeni kusikilizia kama salamu zimefika au laa.

Safari hii salamu zake zilifika bila wasiwasi kabisa. Timu vigogo wa Ulaya wakaanza purukushani kuhitaji huduma ya kinda huyo hatari kabisa. Mabosi wa Vilabu kama Juventus, Manchester United na Borussia Dortmund walipigana sana vikumbo pale Molde Norway kutaka saini ya Haaland, mwisho wa siku Dortmund wakashinda vita hiyo.

Kuhusu anayoyafanya huko Dortmund kila mpenda soka anayo habari. Hakuna kinda anayezungumziwa kuliko Haaland hivi sasa, na iko wazi kuwa pale Dortmund ni njia yake kuifikia kilele chake ki soka.

Mpaka sasa thamani ya Haaland sokoni ni zaidi ya Paundi milioni 88 ambayo inatazamiwa kuelekea kupanda zaidi hasa ukizingatia kuwa kiwango chake kinazidi kukua siku baada ya siku, dogo bado hajavunja undugu wake na nyavu na anazidi kutupia kama kawaida.

Pengine Wengi wanajiuliza undugu wa Haaland na nyavu ulianzia wapi, haukutoka mbali. Ni undugu wa upande wa baba, Haaland ni mtoto wa mchezaji wa timu za Nottingham Forest, Leeds United na Manchester City Alf-Inge Haaland. Baba yake nae ameuchez sana mpira, akamuachia dogo aendeleze undugu usivunjike.

Na ni katika kipindi hicho mzee Alf-Inge Haaland akikipiga katika vilabu vya Uingereza ndipo alifanikiwa kumpata kijana Erling Haaland. Na kwa kuwa dogo alizaliwa nchini Uingereza alikua na uwezo wa kuchagua kuchezea timu ya taifa ya Uingereza, lakini yeye aliamua kuwa mzalendo kwa kuchagua kuichezea timu yake ya asili ya Norway.

Hata huko katika timu ya taifa ya Norway kuanzia ngazi ya vijana alipoanza kucheza, kuanzia timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 15, kisha chini ya miaka 20 mpaka ile timu ya taifa ya wakubwa aliyoyafanya sio madogo.

Timu ya vijana wa chini ya miaka 20 ya Poland habari ya Haaland wanayo, na pengine wanaweza kukusimulia vizuri kabisa kuliko hata watu wa karibu wa dogo mwenyewe. Unajua ni kwanini? Katika mashindano ya kombe la dunia la vijana wa chini ya umri huo mwaka 2019 aliwacharaza magoli 9 katika ushindi wa magoli 12-0 wa vijana wa Norway. Bado una shaka na undugu wa dogo na nyavu? Undugu huu hauhitaji vipimo vya DNA ili kuthibitishwa.

Kwa mtu asiyemfahamu Haaland, baada ya kusoma hizo rekodi zake anaweza kudhani kuwa Haaland ni pande la mtu, la miraba minne labda. Lakini kumbe ni jamaa mmoja mdogo mdogo tu tena aliyezaliwa July 21 mwaka 2000! Sijakosea, ni mwaka 2000 ndiyo. Yani mwaka huu mwezi wa saba dogo anatimiza miaka 20! Huyo sasa ndiyo Erling Braut Håland (sema Haaland) mkaka mwenye future yake.

19 Komentara

    Tatizo la hawa madogo wakishaanza kulipwa mishara mikubwa mpira unawapotea miguuni mfano januzaj

    Jibu

    Yuko poa

    Jibu

    Hilo Ni tatizo
    Wanatakiwa waw na msimamo

    Jibu

    Haaaaaaa hao wenye future sikuhizi wanitwa danga kwaiyo kijana ni dangaa teheteheteheee😁😁😁😁😁

    Jibu

    Erling Haaland 😀😀😀😀, Mkaka Mwenye ‘Future’ wenzetu wameandaliwa kufanikiwa angekuwa bongo tz angebaki story wadaa wange mdangiaa mpaka basis…..

    Jibu

    Vijana km hao wanatakiwa waende kucheza man u.

    Jibu

    Kijana mwenzetu bigup

    Jibu

    Vijana km hawa wakishapata mafanikio wanalewa sifa

    Jibu

    Hata ukikaa na mtu mwenye future nawe utakuwa mwenye future zaidi.
    Kwa hiyo huyo kijana namkubalii sanaa

    Jibu

    dogo anamalengo yakufika mbali.

    Jibu

    Namkubali sanaa huyo kaka

    Jibu

    Kijana yuko vzur sanaa

    Jibu

    Sio kila shalobaro hana future

    Jibu

    Ukiwa na future usharo utakuja tu wnyw kuliko ukawa sharo bila future ufiki mbali kimaisha

    Jibu

    Nakubali Sana brother

    Jibu

    Ufundi wake ndio future ya maisha yake

    Jibu

    Kujituma na kujielewa kwako kutakufanya ueshimike kila sehemu bila ya kunyooshewa vidole

    Jibu

    hii inatakiwa na kila mmoja kutazama mbele ili kujituma zaidi

    Jibu

    Hongera Sana earling halaand ndivyo maisha yanavyotakiwa lazima uwe na future yako ya mbel ya maish yako

    Jibu

Acha ujumbe