Klabu ya Bayern Munich imekubali tena kupokea kichapo kingine ndani ya ligi kuu ya Ujerumani leo dhidi ya timu ya Heidenheim iliyopanda daraja msimu huu kwa mabao matatu kwa mawili.
Bayern Munich wanapoteza mchezo wao wa tano kwenye ligi kuu ya Ujerumani ikiwa ni muendelezo wa matokeo mabaya ambayo mabingwa hao watetezi wa Bundesliga ambayo wamekua nayo ndani ya msimu huu.Vijana wa Thomas Tuchel ndio walioanza kupata mabao mawili ya haraka kupitia kwa mshambuliaji Harry Kane na Sergr Gnabry, Ikionekana huenda wanakwenda kushinda mchezo huo kwa mabao mengi zaidi kwani mchezo huo ulikwenda mapumziko wakiongoza kwa mabao mawili kwa bila.
Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji Heidenheim wakionekana kuhitaji kusawazisha mabao ambayo walikua wametanguliwa na walifanikiwa kwa kiwango kikubwa, Kwani dakika mbili zilitosha kuwapa mabao yote mawili ambapo dakika ya 50 na 51 mabao ya Sessa na Kleindienst yalitosha kuwarudisha mchezoni.
Bavarians waliendelea kujaribu kutafuta ushindi kwa kufanya mashambulizi ya hapa na pale ambayo hayakuonekana kuzaa matunda mpaka pale dakika ya 79 ya mchezo, Ambapo mshambuliaji Kleindienst akiweka msumari wa mwisho na kupelekea mabingwa watetezi kupoteza mchezo.Klabu ya Bayern Munich mpaka sasa wameachwa kwa alama 13 na vinara wa ligi klabu ya Bayern Leverkusen jambo ambalo linaonesha wazi namna gani wamekua na msimu mbaya, Lakini pia klabu hiyo inatoa taswira mbaya kuelekea mchezo wao wa robo fainali wa ligi ya mabingwa ulaya dhidi ya Arsenal siku ya Jumanne.