Mshambuliaji mkongwe wa Lille, Giroud, ameashiria kwamba anapanga kutundika daluga mwishoni mwa msimu huu baada ya zaidi ya miongo miwili akicheza katika kiwango cha juu.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, ambaye hapo awali alikuwa mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo, alifichua mpango wake wa kustaafu siku moja kabla ya kutimiza miaka 40. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal na Chelsea sasa amedhamiria kufurahia kila mchezo uliosalia wa Ligue 1 kabla ya kufunga pazia la safari yake yenye mafanikio makubwa.
Giroud, ambaye sasa yuko katika msimu wake wa pili Stade Pierre-Mauroy baada ya kujiunga na Lille kwa uhamisho wa bure akitokea Los Angeles FC mwaka 2025, alizungumzia ukaribu wa mwisho wa maisha yake ya soka. Akizungumza na L’Equipe, alisema: “Kama mchezaji, nadhani huu huenda ukawa msimu wangu wa mwisho. Ndiyo maana ninajaribu kufurahia kila wakati.”
Akisisitiza kuridhishwa kwake na kila kitu alichofanikiwa katika soka, mshambuliaji huyo wa zamani wa AC Milan aliongeza: “Nina amani na nafsi yangu na kila kitu nilichokifanya katika maisha yangu ya soka.”
Safari ya soka ya mshambuliaji huyo imejaa mafanikio makubwa, ikiwemo kutwaa kwa kusisimua taji la Ligue 1 akiwa na Montpellier kabla ya kuhamia Arsenal kwa ada ya pauni milioni 12 mwezi Juni 2012.
Baadaye alishinda taji la Ulaya akiwa na Chelsea na kutwaa Scudetto akiwa na AC Milan. Katika kipindi chake chote cha soka la kulipwa katika ngazi ya klabu, mshambuliaji huyo mwenye nguvu na umbo kubwa amefunga mabao 303 katika mechi 806. Katika ngazi ya timu ya taifa, urithi wake umeendelea kuwa imara baada ya kufunga mabao 57 katika mechi 137 alizoichezea Les Bleus.

Giroud bado ana mkataba na Lille hadi mwisho wa msimu huu baada ya kuongeza muda wa kukaa klabuni hapo kwa miezi 12 zaidi. Mshambuliaji huyo amecheza mechi sita katika mashindano yote msimu huu, akifunga bao moja huku mara kwa mara akipokea makofi ya heshima kutoka kwa mashabiki wa timu pinzani katika viwanja mbalimbali nchini Ufaransa.
Changamoto yake ya sasa itakuwa kusaidia kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ili kuwaweka Les Dogues kwenye ushindani wa juu wa Ligue 1, huku pia wakilenga kufanya vizuri na kusonga mbali katika Ligi ya Mabingwa.


