Mwamuzi wa mpira wa miguu kutoka Somalia, Omar Artan, amerejea nyumbani mjini Mogadishu na kupokelewa kwa heshima kubwa kama shujaa licha ya kushindwa kutimiza ndoto yake ya kuchezesha Kombe la Dunia la FIFA 2026 baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini Marekani.
Artan, mwenye umri wa miaka 34, alikuwa amechaguliwa na FIFA kuwa miongoni mwa waamuzi watakaosimamia mechi za mashindano hayo makubwa duniani. “Ilikuwa fursa ya kipekee si kwangu tu bali kwa taifa zima la Somalia,” alinukuliwa akieleza baada ya kurejea nchini kwake.
Bila kusahau meridianbet ndio wakali wa ODDS KUBWA, Machaguo zaidi ya 1000 na kila kitu ukitakacho. Bashiri kijanja hapa
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mwamuzi huyo alizuiwa na mamlaka za uhamiaji alipowasili katika mji wa Miami, licha ya kuwa na pasipoti ya kidiplomasia pamoja na visa halali ya Marekani. “Nilifuata taratibu zote zinazohitajika, lakini sikuruhusiwa kuingia nchini,” alisema Artan.
Tukio hilo limezua hisia kali miongoni mwa wadau wa soka nchini Somalia na Afrika kwa ujumla, huku wengi wakieleza masikitiko yao kutokana na kupotea kwa nafasi ya kihistoria ambayo ingemfanya kuwa mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuchezesha Kombe la Dunia.
Licha ya changamoto hiyo, mamia ya wananchi walijitokeza kumpokea alipowasili Mogadishu, wakimtambua kama mfano wa mafanikio na uthubutu. “Kwetu bado ni shujaa, kwa sababu amefika mahali ambapo WaSomalia wengi hawajawahi kufika katika soka la kimataifa,” alisema mmoja wa mashabiki waliojitokeza kumpokea.


